Serikali Yasema Zuio la wanafunzi wanaopata mimba Kuendelea na Masomo halihusu shule binafsi

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu hatua ya kuzuia wanafunzi wanaopata mimba kurejea shule kuwa suala hilo halizihusu shule binafsi.

Ufafanuzi huo umetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenda kwa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco) ukiwataka kutofuata maelekezo ya awali yaliyotolewa Agosti Mosi, 2017.

Katika barua ambayo imeandikwa kwa Tamongsco na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuthibitishwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo imezitaka shule binafsi kuwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo kwani zuio hilo haliwahusu wao.

“Ni kweli tumewaandikia barua Tamongsco kwani ufafanuzi huo unatokana na maelekezo ya awali kuwachanganya na yalikuwa hayawahusu wao bali shule za umma,” alisema Dk Akwilapo.

Katibu mkuu huyo alisema badala ya maelekezo hayo kuyatuma kwa shule binafsi anuani zikakosewa na kutumwa kwa shule binafsi jambo ambalo limewafanya kuwatumia barua ya ufafanuzi kuwa zuio haliwahusu na wanaweza kuendelea na wanafunzi wanaopata ujauzito na hata Rais Magufuli alisema marufuku hiyo ni kwa shule za umma.

Alipoulizwa kama mwanafunzi atakayekuwa amepata ujauzito katika shule za umma ataruhusiwa kuendelea akihamishiwa shule binafsi, Dk Akwilapo alisema, “Ataruhusiwa na atakwenda kujiunga huko kwa kufuata taratibu ikiwamo kufanyishwa mitihani.”

Julai 22, 2017, Rais Magufuli akiwa Msata wilayani Bagamoyo mkoani Pwani alisema katika muda wote atakaokuwa madarakani hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari atakayepata ujauzito atakayeruhusiwa kuendelea na masomo katika shule za umma.

“Nataka niwaambie, katika utawala wangu hakuna mwanafunzi mwenye mimba atakayerudi shuleni. Yapo mambo mengi ya kufanya, wanaweza kwenda Veta au wakajifunza kushona, maisha yakaendelea,” alisema Rais Magufuli

Credit: Mwananchi


from MPEKUZI

Comments