Serikali ya Misri yawasilisha andiko la kwanza la nia ya kuwekeza nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amefanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Misri hapa nchini Bibi. Nevine El-Saeed pamoja na kupokea andiko la awali la nia ya serikali ya Misri kutaka kuwekeza nchini katika sekta ya mifugo.

Kaimu Balozi wa Misri ambaye ameambatana na Mkuu wa Idara ya Uchumi katika ubalozi huo Bw. Mohamed Ibrahim katika ofisi ndogo za wizara ya mifugo na uvuvi zilizopo jijini Dar es Salaam, amesema serikali ya nchi hiyo inahitaji kuwekeza ili kufungua fursa mbalimbali ambazo zitapatikana kupitia uwekezaji huo.

Akizungumza na maafisa hao pamoja na wajumbe waliohudhuria kikao hicho, Katibu Mkuu Ole Gabriel amesema nchi ya Tanzania ina mifugo mingi na kwamba ikitumika vizuri kupitia uwekezaji, ambapo nia ya serikali ya awamu ya tano imejikita zaidi kupitia kufufua na kuanzishwa kwa viwanda vipya kutaongeza fursa nyingi zaidi zikiwemo za ajira.

Aidha, amesema nia yake ni kuhakikisha anasimamia nia ya serikali ya Misri kufanikisha uwekezaji huo ambao anasema wizara yake itahakikisha inaweka mazingira yatakayofanya uwekezaji huo uwe endelevu na kuleta tija kwa nchi zote mbili.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na wakuu wa idara zilizo chini ya ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wawakilishi kutoka Dawati la Sekta Binafsi, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Kituo cha Kuendeleza kilimo Nyanda za juu Kusini (SAGCOT) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki.


from MPEKUZI

Comments