Rais Magufuli: “Lowassa washauri unaowaongoza la sivyo wataishia Gerezani”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amempongeza Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa kwa kitendo cha kuhudhuria kuungana na serikali katika miradi ya maendeleo.

Rais Magufuli amefunguka hayo wakati akihutubia katika uzinduzi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambapo amesema kuwa pamoja na kumshinda katika uchaguzi mkuu wa 2015 lakini bado hakuwa na kinyongo nae na kukaa kimya huku wasiohusika wakipiga kelele.


 “Siku zote huwa nasema, Lowassa umekomaa kisiasa, ndio maana unahudhuria katika shughuli za kimaendeleo, maendeleo hayana, chama, kabila, dini, wala rangi.

“Nakupongeza sana Lowassa kwa utulivu wako, Wewe ndo tuligombea Urais lakini nilipokutupa chini ukaenda ukapumzika Mzee wa watu wenye kelele wengine hata hawakugombea, Wewe unajua ktk mashindano yoyote kuna kushindwa.

“Vyama vyetu kamwe visiwe chanzo cha kututenganisha, nimeona nizungumze kwa heshima kubwa Mzee Lowassa ili wale unaowaongoza kule angalau ukawashauri otherwise wataishia kwenye Magereza”
,- Rais Magufuli


Hadi sasa, viongozi kadhaa wa upinzani, hasa Chadema waka kesi za aina tofauti katika mahakama mbalimbali nchini; baadhi wakishtakiwa kwa uchochezi, wengine kwa kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais na wengine kwa kufanya mikusanyiko bila ya kibali.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifutiwa dhamana pamoja na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana katika kesi inayowakabili ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria.

Lakini Lowassa, ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi za juu kujivua uanachama wa CCM na kujiunga na upinzani, hajawahi kukumbwa na matatizo dhidi ya mamlaka, zaidi ya kuitwa kituo cha polisi kutoa maelezo.

Lowassa alihamia upinzani mwaka 2015 akipinga kitendo cha Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake na la wagombea wengine wa urais na kujiunga na Chadema, ambayo ilimpa fursa ya kutimiza ndoto yake ya kugombea urais.

Katika harakati zake, Lowassa aliungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioundwa na Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi na kushika nafasi ya pili, akiwa ameweka rekodi ya upinzani kupata kura nyingi. Alipata kura milioni 6.7, akiwa nyuma kidogo ya Rais Magufuli, aliyepata kura milioni 8.8.


from MPEKUZI

Comments