Katibu Mkuu Wizara ya Habari Akagua Mendeleo ya Maboresho ya Uwanja wa Taifa kwa Ajili Mashindano ya AFCON U17

Na Eliphace Marwa- WHUSM, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bibi.Susan Mlawi amemtaka mkandarasi anayeboresha Uwanja wa Taifa kuhakikisha anamaliza kazi kwa wakati kuelekea mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 yanayotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2019.


Bibi. Susana ametoa kauli hiyo hivi karibuni Jijini Dar es salaam alipotembelea uwanja huo lengo ikiwa ni kuangalia na kukagua maboresho yanayoendelea katika uwanja huo chini ya usimamizi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group. Co Ltd.


“Ni heshima kubwa tumepewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika kwa kuwa waandaaji na wenyeji wa mashindano haya makubwa ni vema mkamilishe kazi hii kwa wakati ili kufanikisha mashindano hayo” alisema Katibu Mkuu Bibi. Susan Mlawi.

Aidha kwa upande wa Mkandarasi toka Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group. Co Ltd. Bw. Zhang Jiawa amemuhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa kazi hiyo ya maboresho itakamilika kwa wakati na kuahidi kuwa anatarajia kukabidhi kazi hiyo mapema mwanzoni mwa mwaka 2019 kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

“Nahaidi kuwa ifikapo mwezi Februari mwaka 2019 kazi uliyonipa ya kuboresha uwanja huu itakuwa imekamilika , tayari kwa kufanya mashindano hayo” alisema Bw. Zhang Jiawa.

Naye Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Nsajigwa Gordon amemuhakishia Katibu Mkuu kuwa anaridhishwa na kasi ya maboresho yanayoendelea kufanyika katika uwanja huo.

“Naomba nikuhakikishie Katibu Mkuu kuwa kazi inayoendelea kufanyika inaridhisha na mkandarasi anafanya kazi kwa kasi ili kuweza kuimaliza kwa wakati na kuweza kufanikisha mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 yatakayofanyika mapema mwakani”, alisema Bw. Nsajigwa.

Mashindano ya kombe la Mataifa ya Afrika chini ya miaka 17 yanatarajiwa kufanyika hapa nchini mapema mwezi Aprili mwakani na kushirikisha nchi nane


from MPEKUZI

Comments