Wizara Zakutana kujadili Kamera za kudhibiti Uhalifu

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zimekutana kujadili ufungaji kamera maalumu za kudhibiti na kuzuia uhalifu.

Akizungumza wakati wa kikao hicho jana mjini hapa, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema serikali inatambua umuhimu wa ulinzi na usalama kwa raia wake na iko katika mpango wa kufunga kamera hizo katika miji yote mikuu nchini.

Masauni alisema lengo la kufunga kamera hizo ni kuiwezesha serikali kupambana na matukio ya uhalifu ya utekaji, makosa ya barabarani, uporaji wa fedha katika taasisi za fedha.

“Tumekuja kuchukua uzoefu kwa wenzetu wa Zanzibar ambao tayari wameshafunga kamera hizi katika maeneo mbalimbali na nimeona jinsi zinavyofanya kazi za kubaini wahalifu.

“Teknolojia haiepukiki katika kudhibiti, serikali tumejipanga na hivi karibuni tutaanza kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu na maeneo ya mikoa iliyoko mipakani ili kudhibiti wahalifu kutoka nje ya Tanzania,” alisema.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Radhiya Rashid Haroub alisema tayari washafunga kamera hizo zilizozinduliwa Oktoba 3, mwaka huu.

Alisema uzinduzi wa kamera hizo ulifanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. “Mfumo huo ni muhimu na tumehakikisha unaimarisha usalama katika mji wa Zanzibar ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa amani na salama na tayari ushaanza kufanya kazi katika maeneo mbalimbali hapa Zanzibar,” alisema.


from MPEKUZI

Comments