Wazee Wamfanyia Tambiko Dr Kigwangalla

NA ANDREW CHALE, NZEGA
 WAZIRI wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbao la Nzega Vijijini la Mkoani Tabora, Dkt. Hamisi Kigwangalla amewashukuru viongozi mbalimbali wa dini Nchini kwa dua na maombi yao kwa kipindi chote alichopata ajali hadi sasa kupona na kurejea tena na majukumu yake.

Akizungumza katika mkutano wake wa pili uliofanyika katika Kata ya Lusu Tarafa ya Nyasa iliyopo kwenye jimbo lake hilo la Nzega Vijijini, jana Oktoba 28, 2018,  Dkt. Kigwangalla amewashukuru viongozi hao wa dini pamoja na Wazee wa Mila kwani wao wamekuwa chachu kwenye kupona kwake tokea alipolazwa Hospitali kwa zaidi ya miezi miwili kwa kuuguza majeraha ya mwili wake kutokana na ajali ya gari aliyopata Agosti 4, mwaka huu.

Amesema viongozi wa hao wa dini pamoja na  Wananchi kila mmoja kwa nafasi yake walikuwa ni wa kipekee na dua zao zimeweza kusaidia  na kwa sasa amerejea kutoa shukrani na kupokea dua zao hizo kwani kwa sasa ameanza kufanya kazi.

“Kwa sasa nimeanza kurudi kwenye majukumu yangu kama kawaida. Kwa hivyo nikaona kabla ya kuanza kuonekana nikiruka huku na kule kwenye majukumu ya kiwizara, nikasema hapana nirudi kwanza nyumbani nipate dua za wazazi wangu, dua za wazee na viongozi wa dini.

Kwa tukio lile kwa sisi tunaoamini,  ni mkono wa Mungu ulikuwa mahala pale” amesema Dkt. Kigwangalla.

Aidha, Dkt. Kigwangalla amewatoa hofu wananchi wa jimbo lake juu ya watu waliokuwa wakipitapita jimboni kwa lengo la kulinyemelea na kutoa maneno ya kumkatisha tamaa.

“Kwa waliokuwa wanatembea na wakikesha usiku kucha wakisubiri nife wameanguka. Mungu amesimama  mbele yangu, mimi ni mzima naendelea kutekeleza majukumu yangu mdogomdogo mpaka nitakapokuwa imara kabisa. Sasa naanza upya” amesema Dkt. Kigwangalla.

Pia amewahakikishia wananchi hao kuwa kazi za maendeleo ya jimbo hilo zinaendelea na wasaidizi wake wa ofisi ya Mbunge inaendelea kuratibu kwa ukaribu kabisa na  milango ipo wazi.

Katika hatua nyingine Wazee wa Mila na Watemi wakiongoza na Chifu Ng’wana Ng’washi wa Wasukuma walifanya tambiko la kichifu la kumtambikia ili akawe tayari kwa kazi za kulitumikia Taifa katika majukumu ya Kibunge na Uwaziri.

 Dkt. Kigwangalla yupo katika ziara ya kutoa shukrani na dua maalum kwa Wananchi wa jimbon lake hii ni tokea kurejea kutoka kuuguza majeraha ya mwili wake tokea kupata ajali Agosti 4, mwaka huu wakati akiwa katika majukumu yake ya kikazi Mkoani Manyara.


from MPEKUZI

Comments