Waliopoteza Ajira Kupata Mafao Yao Mwezi Ujao

Mamlaka  ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imesema mifuko ya PSSSF na NSSF iko katika hatua za mwisho za kujenga mifumo ya ndani ya ulipaji wa fao la upotevu wa ajira, maarufu Fao la Kujitoa.

Vilevile, imesema Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), utaanza kupokea maombi ya fao la upotevu wa ajira kuanzia Novemba Mosi, mwaka huu (Alhamisi), likiwalenga waliopoteza ajira baada ya sheria kuanza kazi Agosti Mosi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa sheria mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, kutakuwa na mifuko miwili nchini ambayo ni PSSSF inayohudumiwa watumishi wa umma ambayo ni muunganiko wa mifuko ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF.

Pia kuna mfuko wa NSSF ambao unahudumia wafanyakazi wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.

Hayo yalisema jana na Meneja Mawasiliano wa SSRA, Sara Kibonde, alipozungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua kama mifuko hiyo imeshaanza kutoa fao la upotevu wa ajira ambalo limetajwa katika sheria mpya ya mfuko wa hifadhi ya jamii.

"Kukosekana kwa utaratibu wa kinga ya kipato kwa wafanyakazi wanaopotea ajira kumesababisha wafanyakazi kujitoa uanachama na kuchukua michango yao, ili kujikimu baada ya kupoteza ajira kiasi cha kupewa jina la fao la kujitoa na hiyo ilitokana na kukosekana kwa mbadala wake," alisema.

Kwa mujibu wa Kibonde, ukuaji wa sekta binafsi umechangia kuwa na mabadiliko katika soko la ajira na kuchangia ongezeko la fursa za ajira zenye masharti ya muda mfupi ya ajira na kusababisha wafanyakazi kuomba kujitoa uanachama katika mifuko ya hifadhi ya jamii mara mikataba yao ya ajira inapokoma.

Alibainisha kuwa takwimu zinaonyesha wafanyakazi walio kwenye kundi la masharti ya ajira za kudumu ndiyo lina matukio mengi ya wanachama kujitoa.

"Kuwapo kwa idadi kubwa ya wafanyakazi wanaojitoa kutoka kwenye kundi la wafanyakazi wenye mikataba ya ajira ya muda mrefu kunaashiria kwamba baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakijitoa bila sababu za msingi."

Alisema mwanachama anayechukua michango yake anakuwa amepoteza sifa ya kulipwa mafao ya pensheni atakapotimiza umri wa kustaafu na ndiyo maana sheria mpya imeleta utaratibu mbadala ambao utakuwa kinga ya kipato.

Kwa mujibu wa kanuni za sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii ya mwaka 2018, utaratibu wa kujitoa kwenye mifuko hiyo umeainishwa kuwa mafao ya kujitoa yatakuwa asilimia 33.3 ya mshahara wa mwezi wa mwanachama husika.

Pia, muda wa ulipaji mafao ni miezi sita na mwanachama atalipwa kwa kipindi kisichozidi miezi 18 na mwanachama aliyechangia chini ya miezi 18 atalipwa asilimia 50 ya michango yake.

Kanuni hizo pia zinabainisha kuwa kama mwanachama atakuwa hajapata ajira baada ya miezi 18, atamwandikia Mkurugenzi Mkuu wa mfuko kuomba kuhamishia michango yake kwenye mfuko wa hiari na kuendelea kuchangia.



from MPEKUZI

Comments