TAKUKURU Yawafikisha Mahakama Vigogo ACACIA Kwa Rushwa ya Bilioni 13.5/-

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Mara, imewafikisha mahakamani watuhumiwa saba akiwamo raia wa kigeni wa mgodi wa North Mara Gold Mine ulio chini ya kampuni ya Acacia kwa kosa la rushwa ya Sh. bilioni 13.5.

Fedha hizo Sh. 11,348,781,535 na Dola za Marekani 925,222 (sawa na Sh. 2,116,850,177), zinadaiwa kutolewa kwa lengo la kuwezesha upendeleo katika uthamini na maamuzi mbalimbali ya vijiji dhidi ya mgodi.

Watuhumiwa hao walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Veronika Mgendi, wakikabiliwa na kesi tano tofauti zinazohusu makosa ya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwenye mgodi huo, kinyume na kifungu 15 (1) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Waliofikishwa mahakamani ni watumishi wa umma ngazi ya uthamini, Adam Yusufu, Peter Mrema na Joseph Kleruu.

Wengine ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, Tanzania Omtima, Diwani kata ya Kemambo, Bogomba Chichake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakunguru, Abel Nyakibaru na raia wa kigeni ambaye ni Mhasibu wa mgodi huo, Marten Vande Walt.

Akisoma hati ya mashtaka, Mwanasheria wa Takukuru, Leonard Swai, alidai kuwa watuhumiwa hao walikula njama za kutenda makosa hayo kati ya Januari 2016 hadi Mei 2018, kwa nyakati na siku tofauti.

Alidai kuwa Diwani Rashid kwa kipindi hicho alijipatia zabuni mbalimbali kwenye mgodi huo kwa njia ya rushwa iliyomwezesha kupata Sh. 7,709,575,914.19.

Swai alidai kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, Tanzania O’mtima alijipatia Sh. 1,102,880,803 alizopokea kutoka mgodi wa North Mara kama kishawishi ili shule ya Nyabigina isihamishwe kutoka Mrwambe kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na badala yake ijengwe Mrwambe kwa unafuu wa gharama kwa mgodi wa North Mara.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Mwenyekiti wa kijiji cha Nyakunguru, Nyakibari alipokea rushwa ya Sh. 966,687,343 iliyolipwa kwake kama fidia kutoka mgodi wa North Mara ili kumshawishi kusaidia mgodi huo kutowalipa baadhi ya wanakijiji fidia.

Alidai mahakamani kuwa, Mthamini Mkuu na Mshauri wa serikali kwa mambo yanayohusu uthamini, Kleruu katika kipindi cha mwezi Mei na Juni 2013, alipokea rushwa ya Dola za Marekani 243,650.75 (Sh. bilioni 2.1) kutoka North Mara kama kishawishi cha kuwapa upendeleo mgodi huo katika uthamini wa mazao na mali za wananchi na hivyo kuwakandamiza wananchi wanaozunguka mgodi.

Alidai, kutokana na hali hiyo mtuhumiwa aliwapa ahueni isiyo halali wamiliki wa mgodi huo.

Swai alidai kuwa mtuhumiwa huyo akiwa kama Mthamini Mkuu wa Serikali, alijipatia kiasi cha Dola za Marekani, 681,572 (sawa na Sh. bilioni 1.5) kutoka kweye mgodi huo kama kishawishi cha kampuni yake binafsi kupewa kazi ya upimaji na uthamini wa mali na mazao ya wananchi kupisha mgodi huo kuendelea na uchimbaji.

Aidha, alidai O’mtima akiwa Mwenyekiti wa kijiji cha Kewanja, alipokea rushwa Sh. 90,251,475 kutoka katika mgodi wa North Mara, kama kishawishi cha kusaidia mgodi kupata upendeleo katika maamuzi mbalimbali ambayo yatatolewa na serikali ya kijiji.

Aidha, ilidaiwa Welf, ambaye ni raia wa kigeni wa Afrika Kusini, akiwa Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Meneja wa Ardhi wa North Mara Gold Mine, akishirikiana na Johaness Jansen Van Vuuren, ambaye alikuwa meneja kwa pamoja walitoa Sh. 93,896,000 kwa Adam Yususu Adam, aliyekuwa Mthamini Mkuu katika kikosi kazi kama kishawishi cha kutoa upendeleo wa mgodi katika uthamini ambao ungefanywa na kikosi kazi.

Mwanasheria huyo alidai kuwa, Yusumu ambaye ni mthamini mkuu anashtakiwa kwa kosa la kupokea rushwa ya Sh. 93,896,000 kutoka mgodini humo, kinyume cha sheria.

Aidha, Mrema akiwa Mthamini Mkuu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anadaiwa kupokea Sh. 30,000,000 kutoka kwa Johaneness Jansen Van Vuuren, aliyekuwa Meneja wa mgodi kama kishawishi cha kumwezesha awasaidie North Mara kuwapa upendeleo katika uthamini ambao ungeendelea.



from MPEKUZI

Comments