Naibu Waziri Mabula Akagua Majalada Ya Ardhi Serengeti Na Kuwapigia Simu Waliocheleweshewa Hati

Na Munir Shemweta,  WANMM Serengeti
Katika kile kinachoonekana kútekeleza kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya hapa kazi tu,  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula amekagua majalada ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara na kuwapigia simu wananchi ambao majalada yao yana muda mrefu bila ya kupatiwa hati za ardhi.

Akiwa katika oisi ya kutunzia majalada katika halmashauri ya Serengeti  Mabula alikagua jalada moja hadi jingine na kubaini badhi ya majalada yakiwa na muda mrefu huku wananchi wakiwa hawajapatiwa hati ambapo baadhi yake ni za  tangu mwaka 2017 na kumhoji afisa ardhi mteule suala la kuchelewa kuwapatia hati za ardhi pamoja na wahusika kujaza fomu za maombi.

Mabula alielezwa kuwa baadhi ya wananchi wameshindwa kupatiwa hati kwa wakati kutokana na kushindwa kukamilisha baadhi ya taratibu pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanywa na maafisa ardhi wa halmashauri kuwakumbusha jambo lillilomshtua Naibu Waziri kwa kuwa wananchi wengi wamekuwa na  shauku kubwa ya kupatiwa hati.

Katika kujiridhisha na maelezo ya afisa ardhi mteule wa halmashauri ya wilaya ya Serengeti,  Mhe.  Mabula aliamua kumpigia mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Stanslaus na kumuuliza kwa nini hajapatiwa hati katika kiwanja Na 619 kitalu B Chamoto wakati aliwasilisha maombi ya kupatiwa hati.

Mwananchi huyo alipopokea simu na kuelezwa kuwa aliyekuwa akiongea naye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na alikuwa akihoji maombi yake ya hati ya ardhi aliyoyawasilisha  ofisi za halmshauri ya wilaya ya Serengeti,  alishangaa kwa kuwa  muda aliopigiwa simu majira ya saa kumi na mbili jioni  haukuwa muda wa kazi.

Mwanachi huyo mkazi wa Mugumu wilaya ya Serengeti alimueleza Mabula kuwa  alielezwa kuwa hati yake haijafika na yeye hakuelewa kama kuna taratibu hajazikamilisha ili apatiwe hati ingawa alishapatiwa hati za viwanja vingine viwili alizoomba katika halmshauri hiyo.

Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmshauri ya Wilaya ya Serengeti kuhakikisha inawafuatilia waombaji wote wa ardhi na kuwasaidia kuwaelekeza taratibu  zitakazowawezesha kupata   hati zao bila usumbufu wowote.

Alisema,  serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli haitaki kuona wananchi wanasumbuka katika kupatiwe hati za ardhi kwa kuwa hati hizo ni haki yao na zitawasaidia katika shughuli zao za kiuchumi hivyo alitaka wahusika wafahamishwe kwa njia ya simu pamoja na barua kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawa.

Aakikagua  majalada ya ardhi katika halmshauri ya Serengeti, Mabula alibaini utunzaji wa majalada usiofuta taratibu na kuamuru watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha taratibu zote katika kushughulikia  majalada ya ardhi ikiwemo maelekezo kutoka afisa mmoja kwenda kwa mwingine yanazingatiwa ili kuepuka ujanja unaoweza kufanywa katika majalada hayo na kuleta usumbufu kwa waombaji hati.

-----------MWISHO------------


from MPEKUZI

Comments