Miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Julius Nyerere: Butiku Alia na Katiba Mpya

Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema ni vyema yakawepo mabadiliko ya Katiba kwa sababu wananchi hawaridhishwi  na mambo yanayoendelea katika chaguzi mbalimbali nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 12, 2018 akichangia mjadala katika mdahalo wa kumbukizi ya miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Julius Nyerere.

Mdahalo huo uliopewa jina la ‘mienendo ya chaguzi na mustakabali wa mataifa ya Afrika’, umehusisha wanasiasa, wasomi wa watu wa kada mbalimbali.

Butiku amesema kila mara baada ya wananchi kupiga kura kunakuwapo na vurugu zinazosababishwa na viongozi ambao wanajulikana, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Ipo haja ya kuitizama Katiba Mpya ili kujirekebisha kutokana na mienendo ya uongozi iliyopo,” amesema Bujiku.

Amesema binadamu wana hulka ya kujitutumua, kupenda vyeo na kwa kawaida wanapokuwa wengi kunakuwa na utaratibu wa kuwaongoza.

“Katiba iliyokubaliwa na wananchi baadaye ikapelekwa kwenye Bunge Maalumu, ndio ina majibu ya maswali yote haya, ”amesema Bujiku.

Kwa upande wake, Prof Alexander Makulilo Kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam amesema Uchaguzi siyo njia pekee ya kuimarisha demokrasia bali ni njia ya kuondoa uongozi wa mabavu (Udikteta)

"Tumefanya chaguzi nyingi katika bara la Afrika ,lakini suala la msingi je chaguzi hizi zimekuwa za halali na zisizokiuka haki za binadamu? Jibu ni hapana hivyo lazima tuhimize mabadiliko ya katiba yatakayolinda haki za watu na kufuata misingi ya sheria"  Amesema Prof Alexander Makulilo

Prof Musambayi Katumanga kutoka Nairobi Kenya yeye amesema kuwa Nchi nyingi za Afrika zinatumia fedha nyingi kwenye chaguzi badala ya kutumia rasilimali hizi kunufaisha watu wake, hivyo akapendekeza mataifa ya Afrika  kuja na ajenda za kitaifa zitakazolenga kuwanufaisha watu wake na siyo katika kutafuta vyeo

"Uchaguzi kwa sasa imekuwa vita baina ya wanaotafuta madaraka na jamii ambayo inatafuta kiongozi, mara nyingi viongozi wetu wamekuwa wakipigana vita hii bila kujua kama wanakiuka miiko ya demokrasia" Amesema Prof Musambayi Katumanga na kuongeza; 

"Demokrasia siyo adui wa watu wa Afrika lakini adui mkubwa wa waafrika ni uchaguzi jambo amabalo limekuwa likileta migogoro na kuondoa uwezekano wa kujenga taifa imara"


from MPEKUZI

Comments