Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali Yapewa Siku 14 Zaidi Kuwasilisha Taarifa Za Miradi Na Matumizi Ya Fedha Za Mwaka 2016 Na 2017

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa siku kumi nne zaidi (14) kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuhakikisha yanawasilisha taarifa za miradi na za fedha za mwaka 2016 na 2017 zilizokaguliwa kwa Msajili wa Mashirika hayo kabla ya kufutiwa usajili wao.

Tamko hilo limetolewa jana jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto- Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Ufafanuzi ulitolewa kuwa, “Siku ya tarehe 28 Septemba, 2018, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile alikutana na wawakilishi wa vyombo vya habari na kutoa maagizo yakuyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwasilisha taalifa zao kwa Mashirika hayo ikiwa ni pamoja na taarifa za miradi na taarifa za fedha zilizo kaguliwa kwa mwaka 2017 na 2018”, alibainisha DKT. Jingu.

Dkt Jingu amefafanua kuwa, maagizo hayo yalipaswa kutekelezwa ndani ya siku thelathini (30) kuanzia tarehe 28.9.2018 ya agizo lilipotolewa na Serikali. Hata hivyo imeelezwa kuwa mwitikio wa utekelezaji umekuwa wa kuridhisha kutokana na ukweli kuwa Mashirika mengi yamezingatia maelekezo ya Serikali.

Aidha, Wizara imepokea maombi kutoka Ofisi ya Baraza la Taifa la NGOs na baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakiomba kuongezwa muda kidogo ili waweze kukamilisha maandalizi ya taarifa zao na kuziwasilisha haraka. 

Kutokana na kutambua nafasi ya NGOs katika maendeleo ya Taifa, Serikali imeridhia kuongeza siku kumi na nne (14) kuanzia leo (31/10/2018) ili kuwapa fursa wale ambao walikuwa bado hawajatimiza maelekezo hayo kutokana na sababu mbalimbali kufanya hivyo. 

“Nasisitiza kuwa hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza kwa wale ambao hawatakuwa wamewasilisha taarifa hizo ndani ya muda wa nyongeza. Shirika ambalo litakuwa halijawasilisha taarifa Wizara itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria”. alisisitiza Dkt. Jingu.

Katibu Mkuu huyo amerudia kuhakikishia umma kuwa, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa NGOs kwa maendeleo ya nchi. Msisitizo wa Serikali wa uwazi na uwajibikaji unalenga kuwezesha Serikali, wananchi na wadau wa maendeleo kutambua vizuri zaidi mchango wa NGOs  katika shughuli za maendeleo.

 Pia kama ilivyo kwenye sekta nyingine, uwazi na uwajibikaji utasaidia kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali zinazotolewa na wadau wa maendeleo kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuwa kichocheo katika kufikia azma ya maendeleo jumuishi.

Akizungumza katika Mkutano huo, katibu Mkuu wa Braza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bw. Ismail A. Suleiman ameishukuru Serikali kwa kuridhia ombi nyenyekevu la kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa za fedha na miradi ili  kuwezesha NGOs kutimiza takwa la  agizo hio.

Bw. Ismail amebainisha kuwa kanuni mpya za NGOs (2018) zilizotangazwa tarehe 19/10/2018 kwa kiasi kikubwa zimezingatia utekelezaji wa kanunni za maadili; hivyo Braza la NGOs litaunda kikosi kazi kuzipitia na kutoa maoni kwa lengo la kuboresha utendaji wa NGOs kwa mujibu wa matakwa ya kisheria, kanuni na taratibu.

Baraza la NGOs limewataka wanachama wake wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuhakikisha kuwa wanatekeleza kazi zao kwa mujibu wa katiba za mashirka yao ili kushirikiana na Serikali katika kuchochea ustawi na maendeleo ya watu hususan kunufaisha makundi yote ya kijamii.

Maagizo haya kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanakuja mwezi mmoja baada ya AGIZO LA Serikali kutolewa likizitaka NGOs zote nchini pamoja na mambo mengine kuwasilisha taarifa zao za kazi na matumizi ya fedha ya miradi wanayoitekeleza. 

Imeelezwa kuwa hadi taarifa hii inatolewa zaidi ya Mashirika 2000 yamewasilisha taarifa zao na wengi wanaendelea kuitiki maelekezo hayo.


from MPEKUZI

Comments