Makamu wa Rais agoma kufungua stendi ya mabasi Kibaha

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekataa kuzindua stendi kuu mpya ya Mailmoja Kibaha mkoani Pwani, akiwa katika ziara yake mkoani humo.

Hatua hiyo ameifikia kutokana na kupata wasiwasi wa utekelezaji wa mradi kuwa na baadhi ya mapungufu ambapo amedai baada ya kufanya uchunguzi wiki mbili ama tatu zijazo atakwenda kuuzindua. 
 
Akizungumza katika stand hiyo, Samia alieleza, kuna minong’ono wameisikia kuhusu mradi huo hivyo ni jukumu lake kuibeba na atakapo jiridhisha atarudi kwa mara nyingine  .
 
Hata hivyo, alisema atakutana na mkuu wa wilaya, mkurugenzi na mkuu wa mkoa kuzungumzia suala hilo. 
 
“Msishtuke kwa hili ni kawaida kwa kuchukua hatua za aina hii ili kujiridhisha kwa maslahi ya halmashauri, mkoa na watumiaji kijumla “
 
“Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni sikivu na kusikia malalamiko ya wananchi, tumepata malalamiko kidogo kuhusu stand hii, serikali ni ya uwazi na ukweli hivyo sitofungua stendi “alisisitiza Samia. 
 
Samia alimpongeza mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha, Jennifer Omolo na mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama na wahusika waliohusika kufanikisha mradi huo.
 
Nae waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa -TAMISEMI ,Selemani Jafo alisema yeye kama waziri wapo wataalamu wanaohakiki lakini ameridhishwa na kazi hiyo .
 
“Kwani kila kazi ina changamoto za kibinadamu, hasi na chanya, lakini wamejitahidi  “alisema Jafo.

Jafo alieleza, mradi huo umepata msaada wa mkopo nafuu kutoka bank ya Dunia ambao wamepata fedha za kimarekani dollar milioni 255 .

Alielezea , wanagusa miji 18 na wanachokifanya wanagusa stendi tisa, barabara za miji kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa ya kisasa. 
 
Wakitoa kero ya stand hiyo, madereva pikipiki walidai eneo lililotengwa kwa ajili yao halina sehemu ya kujikinga hivyo kusababisha usumbufu wakati wa mvua na jua. 
 
Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha, Jennifer Omolo alisema katika stendi ndogo ya awali walikuwa wakikusanya ushuru sh. 950.000  kwa siku ambapo sasa wanakusanya sh. milioni 1.6 .
 
Alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni 2.9 na walishamlipa mkandarasi bilioni 2.7 ,stendi hiyo itakuwa na mabanda kumi ya kukatia tiketi, mawakala 40 ,eneo la tax, na wafanyabiashara ndogondogo wanaojiingizia kipato kwa kuuza biashara zao wapo 100 .
 
Samia akiwa katika ziara yake Kibaha vijijini na mjini pia alipata fursa ya kutembelea mradi wa reli ya kisasa ya standard gauge kujionea namna unavyoendelea.


from MPEKUZI

Comments