Kada wa CCM mahakamani kwa kuishi nchini bila kibali

Idara ya Uhamiaji, imemfikisha mahakamani Kada maarufu wa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Iringa, Michael Mlowe kwa tuhuma za kuishi nchini bila kibali na kutoa taarifa za uongo kuhusu uraia wake.

Mlowe ambaye kwa jina maarufu Mayko Namlowe (44) ni raia wa Uingereza, alifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Novatus Mlay alidai mshtakiwa huyo ni mfanyabiashara na Mkazi wa Lugalo Kihesa Iringa.

Mshtakiwa anadaiwa kwamba Mei 31, mwaka huu katika Makao Makuu ya Ofisi ya Uhamiaji iliyopo Wilaya ya Temeke akiwa raia wa Uingereza aliishi nchini akiwa hana Visa wala nyaraka yoyote inayomwezesha kufanya hivyo.

Mlay alidai katika shtaka la pili, Mlowe anadaiwa kutoa taarifa za uongo, inadaiwa Mei 31, mwaka huu katika ofisi hizo za uhamiaji akiwa raia wa Uingereza alitoa taarifa ya uongo inayohusiana na uraia wake.

Kwa kufanya hivyo mshtakiwa alijipatia kitambulisho cha kitanzania namba 19741219_51108_00001_24 ambacho kina jina la Michael Juma Mlowe wakati akijua alichokifanya ni kosa.

Mshtakiwa alikana mashtaka, yuko nje kwa dhamana hadi Novemba 11 kesi itakapotajwa.


from MPEKUZI

Comments