Waziri Mwakyembe Awataka Wasanii wa Filamu kuthamini kazi Zao

Na Anitha Jonas – WHUSM – MWANZA
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wasanii wa filamu nchini kutambua thamani ya kazi zao za filamu.

Mheshimiwa Mwakyembe  ametoa agizo hilo leo jijini Mwanza alipokuwa akizindua filamu ya BROTHER  iliyotengenezwa na wasanii wa filamu wa mkoa huo kwa kushirikiana na msanii mkongwe wa filamu Bi.Johary Changula.

“Kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri mliyofanya nimeanza kuona mabadiliko katika tansia hii sasa, kuna mabadiliko makubwa katika upande wa sauti, mwanga na hata namna ya uigizaji ongezeni bidii mkiendelea hivi mtapata mafanikio makubwa na pia msipende kuuza kazi zenu nje kwa bei chini tofauti kazi za nchi jirani,”alisema Dkt.Mwakyembe.

Akiendelea kuzungumza na Waziri Mwakyembe aliupongeza uongozi wa ukumbi wa Sinema wa Misterious wa jijini Mwanza kwa kutenga siku mbili ambazo ni Ijumaa na Jumamosi kwa ajili ya kuonyesha filamu za Kiswahili kutoka ndani ya nchi hii ni hatua kubwa ya uthubutu ningependa kuona na kumbi zote nchini zinaiga mfano huo.

Aidha,Nae Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi.Joyce Fissoo alifafanua kuhusu  changamoto ya upatikanaji wa stempu za TRA kwa kazi za filamu kwa kusema kuwa tayari serikali imeshaanza  kulishughulikia suala hilo kwa kuaandaa nakala laini ya stempu hizo zitakazo sambazwa katika ofisi za TRA mikoani ili kuondoa kero hiyo.

“Kufuatia maombi yenu ya kuitaka ofisi yangu ije tena kwa ajili ya kutoa elimu ya uandaaji wa kazi za filamu basi tutajipanga na tutahitaji kuona wadau wengi wakifika ili tuweze kuhakikisha wadau wa filamu wanaanda  kazi bora mara baada ya kupata elimu ya uaandaji wa miswada ya filamu,”alisema Bibi.Fissoo.

Pamoja na hayo Katibu Mtendaji huyo aliendelea kusisitiza kuwa ukaguzi wa kazi za filamu kwa mikoani upo kisheria chini ya bodi ya filamu katika Halmashauri ambapo inaongozwa na Afisa Utamaduni hivyo siyo lazima kazi ya filamu ipekwe katika ofisi za Bodi ya Filamu Dar es Salaam kwa ukaguzi.

Halikadhalika nae Mwenyekiti wa Chama cha Waandaji wa Filamu Mkoa wa Mwanza Bw.Abdallah Mohamed  alimweleza Waziri Mwakyembe kuwa umoja huo unatarajia kujenga jego la uandaaji wa kazi za filamu kwa kushirikiana na wawekezaji.


from MPEKUZI

Comments