Waziri Mpango Awaonya Watumishi Wa Tra Wasiotaka Kubadilika

Na Benny Mwaipaja, WFM, Tanga
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, kuwachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu wafanyakazi wake wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa na kutumia njia zisizokubalika wakati wa kukusanya kodi za Serikali.

Dkt. Mpango ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TRA Mkoa wa Tanga, ambapo ameagiza wafanyakazi wawili wa mamlaka hiyo, Robinson Munisi na Abraham Maleko waondolewe kwenye kazi wanazofanya sasa na kupangiwa kazi nyingine baada ya kuwepo kwa tuhuma za ulevi wa kupindukia na kujihusisha na mtandao wa wafanyabiashara unaotumika kuikosesha Serikali mapato yake

Amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kuwa waadilifu kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na lugha za kuudhi kwa wateja wao ili kupunguza malalamiko kutoka kwa walipa kodi na kuonya kuwa serikali haitomvumilia mtumishi yeyote atakayefanya kazi kinyume na maadili ili kujenga nidhamu kwa watumishi hao na hatimaye kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato ya Serikali.

“Mwambieni Kamishna Mkuu wa TRA (Bw. Charles Kichere) kwa watumishi hawa siwataki, wapelekeni maeneo mengine mbali huko na muendelee kuwachunguza, na nataka kupata taarifa ya watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kujihusisha na rushwa” alisisitiza Dkt. Mpango

Aidha, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles Kichere, kuhakikisha boti la doria katika Mwambao wa Bahari mkoani Tanga linapatikana haraka ili kuzuia biashara ya magendo inayoyofanywa kwa kutumia bandari bubu hivyo kuikosesha Serikali mapato yake.

“Ni lazima jambo hili lifanyike haraka kwa sababu ya umuhimu wake kwasababu si tu kwamba Serikali inapoteza mapato yake kutokana na vitendo hivyo vya kuvusha magendo kupitia bandari bubu lakini pia ni hatari kwa usalama wa Taifa kwa sababu maadui wanaweza kupitisha silaha” alionya Dkt. Mpango.

Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Mamalaka hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Bw. Masawa Masawa alisema makusanyo ya Mkoa huo yamekuwa yakiongezeka Mwaka hadi Mwaka kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka 2013 hadi 2017 ambapo katika Mwaka 2016/17 Mkoa ulikusanya Shilingi bilioni 107.39 kati ya Shilingi bilioni 131.06 ya malengo kwa Mwaka huo ambayo ni sawa asilimia 82 ya makusanyo. 

Kuhusu maadili ya wafanyakazi wa Mamlaka hiyo mkoani Tanga, Bw. Masawa amesema kuwa pamoja na kuwapa elimu kuhusu maadili mema kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU, wamekuwa wakiwachukulia hatua kali watumishi wao wanaobainika kujihusisha na vitendo vinavyochafua taswira ya mamlaka hiyo.

Akihitimisha mkutano huo, Dkt. Mpango, alimwagiza Meneja huyo kupandisha kiwango cha ukusanyaji mapato kwa asilimia 100 na kutoa onyo kwa Mameneja wote wa TRA nchini watakaoshindwa kufikia lengo hilo wajitathmini kama wanatosha kwenye nafasi zao.


from MPEKUZI

Comments