Serikali Yaanza Kulipa Madai Ya Marejesho Ya Vat Ya Wafanyabiashara Nchini

Na Benny Mwaipaja, WFM, Tanga
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekutana na wafanyabiashara mkoani Tanga na kuwaeleza kuwa Serikali imeanza kulipa  madai ya marejesho ya kodi ya Ongezeko la thamani (VAT Refund) kwa kampuni na wafanyabiashara mbalimbali nchini wakiwemo waagizaji wa sukari za viwandani ambao madai yao yamehakikiwa kuanzia mwezi huu wa Septemba, 2018.

Kauli hiyo ya Serikali inafuatia maombi ya wafanyabiashara wa mkoa huo walioitaka Serikali kuwalipa wafanyabiashara wanaodai kurejeshewa fedha zao zinazotokana na kufanya biashara zao nje ya nchi pamoja na  wazabuni mbalimbali.

Waziri Mpango amesema kuchelewa kulipwa kwa madai hayo kunatokana na kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu hivyo kutaka kuingizia Serikali hasara kwa kulipa madai hewa. ‘Kuna baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu, mfano tulipofanya uhakiki tuligundua madai hewa ya pembejeo ya zaidi ya Shilingi bilioni 87’, alisema Waziri Mpango.

Dkt. Mpango aliwahakikishia wafanyabiashara wote nchini kuwa serikali itahakikisha inaweka mazingira mazuri ili kila mwananchi mwenye nia njema aweze kufanya biashara halali itakayomletea faida na serikali iweze kukusanya kodi bila ya kumuonea mtu.

Awali Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Tanga Bw. Deogratias Ruhinda, alisema kuwa wafanyabiashara hasa wakulima wa zao la Mkonge wanakutana na changamoto kubwa kutokana na serikali kuruhusu na kutoa msamaha wa baadhi ya kodi kwa wafanyabiashara wanaoingiza Kamba za manila hapa nchini, hivyo kulifanya zao la mkonge kutokuwa na soko hapa nchini kutokana na bei ya Kamba hizo za nje kuwa chini ukilinganisha na Kamba zinazotokana na mkonge.

Aidha wafanyabiashara hao waliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza kina cha Bandari ya Tanga ili meli kubwa ziweze kuja  katika bandari hiyo na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa nyingi kutoka Tanga zinasafirishwa kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam au Mombasa jambo linalowaongezea gharama kubwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga.

Akijibu hoja mbalimbali za wafanyabiashara hao, Dkt. Philip Mpango, aliwahakikishia kuwa Serikali itazipitia na kuzitolea ufafanuzi kero zote zinazohusu kodi ili kurahisisha biashara na kuweka mahusiano mazuri kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania, hali ambayo itaongeza mapato kwa serikali. Pia amesema Serikali inalifanyia kazi suala la wingi wa kodi anazolipa mfanyabiashara kwa Taasisi mbalimbali za serikali ili kodi hizo ziweze kutozwa sehemu moja  na kupunguza adha wanazopata walipa kodi.

Waziri Mpango aliwataka wafanyabiashara hao kutosita kuishauri serikali njia bora ya kukusanya kodi na kutoa maoni yao jinsi ya tozo mbalimbali zinazotozwa na serikali kwa kuiandikia Mamalaka ya Mapato Tanzania au Wizara ya Fedha na Mipngo ili serikali iweze kuboresha maeneo yenye mapungufu kwa faida ya Taifa. Pia Mh.Waziri amewataka wafanyabiashara kote nhini kushiriki katika mikutano ya sera za kodi inayondaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango ambayo huanza mwezi Disemba hadi Januari kila Mwaka.



from MPEKUZI

Comments