Serikali Kwa Sasa Inaboresha Maeneo Ya Utawala....Asema Lengo Ni Kuziwezesha Halmashauri Kujiendesha Zenyewe

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano kwa sasa ni kuboresha maeneo ya utawala kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo na kuongeza uwezo wa halmashauri kujiendesha zenyewe.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 27, 2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete, jijini Dodoma.

Ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa maombi mengi ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala nchini. “Kama mnakumbuka nimekuwa nikieleza mara kadhaa kwamba tunazishukuru Serikali za Awamu zilizotangulia kwa kuainisha maeneo ya utawala.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanapaswa wajitathmini sambamba na kuainisha mikakati mizuri ili kuhakikisha lengo la kusogeza huduma kwa wananchi linatimia.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwaka 2014/15 jumla ya halmashauri 66 na mkoa mmoja wa Songwe vilianzishwa pamoja na vijiji 1,949, mitaa 1,379 na vitongoji 8,777. Hadi sasa, maeneo hayo hayajaweza kuwa na miundombinu, vifaa na watumishi wa kutosha ili kuwezesha wananchi kupata huduma iliyokusudiwa.

“Mathalani, mkoa wa Songwe halmashauri zake zote, hata halmashauri ya wilaya ya Mbozi ambapo ndiyo makao makuu ya mkoa bado haujafikia vigezo vya kuwa Manispaa. Baadhi ya halmashauri zinaendelea na ujenzi wa ofisi wakati nyingine kama Mafia, Rufiji, Handeni na Ludewa zipo kwenye magofu na huwezi kuamini kama ni Ofisi za Halmashauri.”

“Taarifa nilizonazo hadi sasa ni kwamba tayari sh. bilioni 120.7 zimepokelewa kwenye halmashauri mbalimbali kati ya sh. bilioni 238.8 zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa majengo ya halmashauri sawa na asilimia 50.54 ya fedha zote.

Amesema kiasi kilichobaki kitaendelea kutolewa kupitia bajeti ya Serikali na mapato ya ndani ya halmashauri, ambapo baadhi yake zitapewa fedha za kukamilisha ujenzi baada ya uhakiki kwa sababu zimekuwa zikipokea fedha kwa muda mrefu.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa halmashauri hizo wahakikishe wanajenga Ofisi za Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji badala ya kuendelea kuanzisha Serikali hizo huku zikiwa hazina hata ofisi.

Kuhusu uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na zoezi la kuajiri watumishi hususan wa kada za afya na elimu, ambapo kati ya mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 Serikali imeajiri watumishi wa kada ya elimu 13,472 na afya 8,238 kwa lengo la kuziba mapengo yaliyopo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments