Serikali Kuendelea Kuwezesha Wananchi Wanyonge Kumiliki Ardhi

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO Dodoma.
Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha wananchi hasa waishio vijijini wanapata haki za msingi za umiliki wa ardhi na makazi nchini.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Mheshimiwa Angelina Mabula wakati wa uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania  mwaka 2017/2018.

“Tunafahamu Watanzania walio wengi na ambao ni masikini wanaishi vijijini na wizara yangu inadhamana ya kusimamia eneo hili, kama Waziri mwenye dhamana nitajitahidi kadri ya uwezo wangu na kuendelea kushirikiana na viongozi wenzangu na wananchi wote kuhakikisha nyaraka rasmi za umiliki ardhi na makazi zinatolewa” ameongeza Dkt. Mabula.

Aidha, akizungumzia kuhusu utoaji wa hati, Dkt. Mabula amesema kuwa kwa sasa utoaji wa hati umeongezeka kwa mujibu wa taarifa kutoka katika Kanda nane nchini.

“Jumla ya Hati 25,463 zimeandaliwa katika Halmashauri mbalimbali nchini, Hati 17,680 zimewasilishwa ofisi za Kanda kwa ajili ya usajili na Hati 9,739 zimeshakamilika” amefafanua Dkt. Mabula.

hata hivyo Dkt. Mabula amesema kuwa, kwa mwaka 2018/2019 Wizara yake imejipanga kuandaa hati za hakimiliki za kimila 120,000 mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji 30 na mpango kina wa vijiji na kupima viwanja 20,000 ikiwa ni kumuwezesha mwananchi kuwa na uhakika na salama ya miliki yake na kuepusha mgogoro.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa utafiti huo umelenga kutoa viashiria mbalimbali kuhusu rasilimali ardhi, nyumba na makazi nchini na kutumika katika kufuatilia malengo yaliyopo katika Mpango kazi wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ijayo, Malengo endelevu ya Maendeleo na Afrika Ajenda 2063.

“Utafiti huu ulifanyika Tanzania Bara na Zanzibar na sampuli ilichaguliwa kwa utaalamu na ilitumika kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 na kuendelea” ameongeza Dkt. Chuwa.

Utafiti wa Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania  kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2016/2017 na wa pili mwaka 2017/2018 na watatu mwaka 2018/2019 unaendelea na ukusanyaji wa taarifa za kitakwimu ambao matokeo yake yatazinduliwa mwaka 2019.


from MPEKUZI

Comments