Rais Magufuli Ataja Sababu Za Kumtumbua Naibu Waziri, Katibu Mkuu Wizara Ya Mambo Ya Nje

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. John Magufuli ametaja sababu za kutengua uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba na kumhamisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Adolf Mkenda.

Akizungumza katika hafla ya kumuapisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk.Damas Ndumbaro  iliyofanyika leo tarehe 29 Septemba 2018 Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema baadhi ya watendaji wa wizara hiyo hasa wakurugenzi wamekuwa wanafanya kazi kwa mazoea.

“Na hili nalirudia, mambo yake pale hayaendi vizuri kama inavyotakiwa kufanya, inawezekana wakurugenzi pale wengi wako weak (dhaifu) sana  au wamezoea, wanajua wanafanya kazi kwa mazoea,” amesema Rais Magufuli .

“Ninasema hivi kwa makusudi ili (Dk Ndumbaro) ukienda huko  usipojua la kufanya halafu likatokea hilo la kutumbua usije kulaumu kwamba sikusema.”

Amesema wizara hiyo imekuwa haitoi ushirikiano hata katika baadhi ya mataifa yanayotuma barua, huku akitolea mfano wa Balozi wa China kutuma barua 24.

“Balozi wa China aliwahi kuandika barua 24 pale (Wizara ya Mambo ya Nje) lakini zikajibiwa mbili, Balozi Kairuki kule China hawajibu.”

Dk Ndumbaro ambaye ni mbunge wa Songea Mjini ameteuliwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa naibu waziri wa wizara hiyo, Dk Dk Suzan Kolimba.

Katika maelezo yake, Rais Magufuli amesema viongozi wa wizara hiyo husafiri nje ya nchi hususani waziri (Dk Augustine Mahiga) ambaye hivi karibuni amemtuma kumwakilisha katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN).

“Tunategemea anapobaki naibu waziri ofisini ndio anakuwa mkuu wa shughuli zote za wizara, anakuwa msimamizi wa mambo yote siyo naibu anayekuwa anaendeshwa  na wakurugenzi,”


from MPEKUZI

Comments