Mzee Mwinyi kuwa Mgeni rasmi Maadhimisho siku ya Wazee Kitaifa jijini Arusha

Rais Mstaafu, Ally Hassan Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani ambayo kitaifa yatafanyika jijini Arusha Oktoba Mosi, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Arusha Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Naftali Ng’ondi, amesema maadhimisho hayo yatafanyika katika Uwanja wa Kumbukumbu wa Sheikh Amri Abeid.

“Kabla ya maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo ‘Wazee ni hazina ya Taifa, tuenzi juhudi za kutetea haki na ustawi wao’, shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwamo uzinduzi wa maadhimisho hayo ambapo wazee watapata huduma za kupima afya, ushauri wa kitabibu yakifuatiwa na kongamano la wataalamu na wadau wa masuala ya wazee.

“Natoa rai kwa jamii kutambua wajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee katika kupata huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na afya, matunzo na ulinzi, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa na Sera ya wazee ya mwaka 2003 inavyohimiza kuwatambua wazee kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa,” amesema.

Akizungumzia upatikanaji wa matibabu bure kwa wazee, Dk. Ng’ondi amesema idadi ya wazee waliotambuliwa na kustahili kupatiwa matibabu bure ni zaidi ya milioni 1.9 kwa mujibu wa takwimu hadi za Machi mwaka huu na kuwa licha ya changamoto ya matibabu kwa wazee, huduma za afya kwa kundi hilo zimeendelea kuboreka.

“Tuliwaagiza maafisa ustawi wafanye tathmini na kuhakikisha wazee waliopitishwa na wanaopaswa kupatiwa matibabu bure wanapatiwa, tumejiridhisha hilo linatekelezeka na tuna mfumo wa ufuatiliaji,” amesema.


from MPEKUZI

Comments