Mtendaji Mkuu TIC , Balozi Wa Denmark Nchini Tanzania Wafanya Mazungumzo Kuhusu Uwekezaji

Na Grace  Semfuko-MAELEZO
MTENDAJI Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geophrey Mwambe amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Einar Jensen.

Miongoni mwa mambo ambayo wamezungumza ni pamoja na wawekezaji wa nchini Denmark kuja kuwekeza kwa kudai Tanzania  kuna mazingira mazuri ya uwekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji Mkuu wa TIC amesema Balozi Jensen amekuwa mdau mkubwa katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji na pande hizo mbili kufanyabiashara.

“Balozi Jensen ni rafiki mkubwa wa biashara na amekuwa akishiriki kikamilifu katika kuandaa mazingira mazuri ya kiabiashara.Tumekuwa tukishirikiana na Balozi Jensen kuratibu za kuwezesha wafanyabiashara,” amesema Mwambe.

Pia amesema Balozi Jensen katika kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanakuwa na soko la uhakika huku akieleza kwamba Balozi amekuwa akihamasisha wawekezaji wa Denmark kuwekeza nchini Tanzania.

Mwambe amesema siku za karibuni amefanya mazungumzo na Balozi huyo na moja ya mambo waliyoyazungumza ni namna ya kusaidia katika mabadiliko ya kimfumo yanayoendelea kufanywa na TIC.

“Balozi amekubali kuisaidia TIC katika mabadiliko ya kimfumo kiutendaji…kama nchi, tumedhamiria kushindana kidunia, tunakuza uwezo wa kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema

Pia wamekubaliana na Balozi Jensen katika kuandaa maeneo ya yaliyopimwa kwa ajili ya uwekezaji.”Nchini kwetu hatuna tatizo la ardhi kwani ipo ya kutosha ila changamoto ipo kupata eneo ambalo limepimwa.

“Hivyo moja ya mipango yetu ni kuhakikisha maeneo ya uwekezaji yanapimwa na mwekezaji anapohitaji eneo inakuwa rahisi kupata.Bolozi amekubali kusaidia katika upimaji wa maeneo,” amefafanua.

Mwambe amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Denmark kuna kampuni kubwa za nchi hiyo ambazo zimejenga viwanda.

Pia amesema kupitia Balozi huyo Denmark kwa sasa kuna mchakato wa  mradi wa umeme wa upepo unaoendelea mkoani Dodoma.

Kwa upande wake Balozi Jensen amesema nchi hizo mbili zimekuwa kwenye ushirikiano mkubwa kwa miaka 50 na kwamba nchi ya Denmark imekuwa ikisaidia katika mambo mbalimbali yanayohusu uwekezaji.


from MPEKUZI

Comments