Lugola Asema Polisi Watoe Dhamana Siku Zote Za Wiki, Saa 24 Bila Wananchi Kuombwa Rushwa

Na Felix Mwagara, MOHA-Kasulu
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku tabia ya baadhi ya askari Polisi kutoza fedha kwaajili ya huduma ya dhamana kwa watuhumiwa waliopo mahabusu katika vituo vya polisi nchini.

Lugola pia alisema dhamana hizo zinapaswa kutolewa saa 24 na siku zote za wiki na sio vinginezo kwasababu vituo vya polisi nchini vinafanya kazi muda wote zikiwemo siku za mapumziko.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Basanza wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma, jana, Waziri Lugola alisema ni marufuku kwa askari yeyote atakayeshindwa kutoa dhamana kwa kosa ambalo lina dhamana.

“Hii tabia sijui imetoka wapi ambayo imejengeka kwa baadhi ya askari polisi, eti mtu akiingia mahabusu ya polisi siku ya Ijumaa ikifika siku ya Jumamosi na Jumapili hawatoi dhamana wakisema dhamana mpaka Jumatatu, hii tabia sio sahihi na ife haraka iwezekananavyo,” alisema Lugola.

Lugola aliwataka wananchi nchini kuhakikisha wanaripoti matukio ambayo yanavunjwa na baadhi ya polisi hao ambao wengi wao wanatengeneza mazingira ya rushwa.

“Kuna tabia ambayo imezoelewa katika jamii, eti kuingia polisi ni bure ila kutoka ni fedha, hii kauli nataka ife, kwasababu nawajua polisi na hawanidanyi kwa lolote, hivyo ole wao ambao watawanyanyasa wananchi kuwaomba fedha,” alisema Lugola.

Lugola alisisitiza kuwa, dhamana ni haki ya mtu endapo hilo kosa linadhaminika hivyo mwanachi yeyote atakaeombwa fedha anapaswa kuripoti tukio hilo kwa viongozi wa polisi ili polisi achukuliwe hatua za kinidhamu.

Aidha, Waziri Lugola aliwataka maaskari wa usalama barabarani kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na si kuwaandikia makosa madereva kwa kuwakomoa endapo magari yao yanamakosa.

“Gari likiwa na kosa liandikiwe faini, hilo sina shida nalo, lakini utakuta baadhi ya askari wanaandika makosa mengi ili watengeneze mazingira ya rushwa, hii ssi sahihi ” alisema Lugola.


from MPEKUZI

Comments