Jokate Mwegelo -Mipaka Ya Jeshi Na Hifadhi Yenye Ulinzi Iheshimiwe

Na Mwamvua Mwinyi,Ruvu
SERIKALI Mkoani Pwani ,imewaasa wananchi kuheshimu mipaka ya jeshi na hifadhi yenye ulinzi pasipo kuingia katika maeneo hayo bila kufuata taratibu ,ili kujiepusha na migongano isiyo ya lazima.
 
Aidha ,imewaasa vijana wanaomaliza mafunzo ya awali ya kijeshi kwa mujibu wa kisheria ,wasitumie ovyo silaha na ulinzi wawapo uraiani bali watumie mafunzo hayo kuwa mabalozi wa uzalendo wa Taifa lao.
 
Akifunga mafunzo ya vijana wa JKT OP Mirerani ,mujibu wa sheria ,katika kikosi cha jeshi 832 JKT Ruvu ,Kibaha ,kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,Mkuu wa wilaya ya Kisarawe ,Jokate Mwegelo alisema, ifahamike maeneo ya ulinzi wa askari yanapaswa kuheshimiwa .
 
“Pale wananchi wanapokuwa wameingia kwenye maeneo hayo ni vema kuwa watiifu wanapotakiwa,kuamriwa ama kuelekezwa jambo la kulifuata iwapo wameingia kimakosa bila kukaidi ” alifafanua Jokate.
 
Hata hivyo ,Jokate ,aliwakumbusha vijana wajilinde na ngono zembe ili kujiepusha na maambukizi mapya ya VVU na magonjwa ya zinaa .
 
“Muwe wazalendo muwe mabalozi wazuri kwa kuipenda nchi yenu na kukataa rushwa “alielezea .
 
Akisoma risala ya wahitimu ,Joakim Jilolo ,aliaahidi kuwa wazalendo na kulitetea Taifa wakati wakielekea kwenye uchumi wa kati .

Nae mwenyekiti wa waliomaliza OP Kambarage ,mwaka 1990-1991 ,Amir Nondo aliwataka vijana  kuwa na heshima na maadili mema .
 
Nondo alisema, serikali kupitia wizara husika inatekeleza mafunzo kwa moyo wa uzalendo kwa vijana waliohitimu kidato cha sita ili waweze kupata malezi bora.
 
Awali kaimu kamanda wa kikosi 832 Ruvu JKT  ,meja James ,alisema walianza mafunzo 25,June 2018 wakiwa na vijana walikuwa 2,871 ,waliomaliza 2,857 ,wavulana 1,805 na wasichana 1,052 ambapo vijana 14 hawakumaliza kutokana na utoro na kukatisha mkataba.
 
Alitaja ,baadhi ya mafunzo waliyowapatia ni ujasiriamali ,nidhamu ,kupenda kazi ,kudumisha uzalendo ,utii ,umoja kwani ni nguzo katika mustakabali wa maisha yao .
 
Meja James aliwaasa ,wazazi na walezi kuielewa shabaha ya serikali ya kufanya mafunzo hayo kwani wapo wanaowakataza watoto wao  .
 
Mwakilishi wa mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa ,Lt Col JS Mlay , aliwashauri wahitimu kutumia elimu ya ujasiriamali ,stadi za maisha waliyopatiwa kwa lengo la kujiajiri ili kujikwamua kimaisha .
 
Alisema ,mafunzo hayo huwaandaa vijana kuwa viongozi bora ,wa Taifa lao siku za usoni ,wenye uzalendo na uchungu wa raslimali za nchi .


from MPEKUZI

Comments