Waziri Mkuu Ahimiza Ubobezi Kwenye Sheria

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuibuka kwa sekta za mafuta na gesi hapa nchini kumeleta haja ya kuwa na wabobezi wa masuala hayo katika taaluma ya sheria. 
 
“Taaluma ya sheria kwa sasa inahitaji kuwepo kwa ubobezi. Imekuwa si rahisi tena kwa mwanasheria kuwa na utaalamu wa kutosha katika maeneo yote ya sheria. Hii inatokana na ukweli kuwa taaluma ya sheria imepanuka na masuala mapya kama vile mafuta, gesi, haki bunifu na makosa ya kimtandao yamekuwa yakijitokeza kila kukicha,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Agosti 15, 2018) wakati akizungumza na wageni mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema uzinduzi wa ofisi hizo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma. “Uzinduzi wa Ofisi unakamilisha uwepo wa mihimili yote mitatu hapa Dodoma. Mahakama Kuu imetengewa ekari 50 na Ofisi za mabalozi zimetengewa ekari 1,800; na wanatakiwa kuanza ujenzi mara moja,” amesema.

Amesema ofisi hizo ni matokeo ya juhudi za makusudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anazochukua katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini na kuimarisha ulinzi wa maliasili na utajiri wa Taifa kwa kuunda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

“Uamuzi huu wa Mheshimiwa Rais unalenga kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata haki zao kwa wakati na pia maslahi na heshima ya nchi vinalindwa kikamilifu,” amesema.

Akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Waziri Mkuu amesema ni matarajio ya kila mwananchi kuwa ofisi hiyo itapanua zaidi wigo wa utendaji wake hadi kufikia ngazi ya wilaya.

“Binafsi naamini kuwa, huu ni wakati muafaka wa kuongeza kasi ya kutekeleza dhana ya utenganishaji wa shughuli za mashtaka na upelelezi. Hatua hii, itapunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vya kubambikiziwa kesi vinavyodaiwa kufanywa na vyombo vya upelelezi. Ofisi hii inategemewa kuwa mkono wa Serikali katika kuhakikisha kuwa vitendo vya ubambikizaji wa kesi vinakoma na kuhakikisha kuwa kesi zinazofikishwa mahakamani zina ushahidi wa kutosha,” amesisitiza.

Kuhusu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu amesema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ndiyo mtetezi na mlinzi namba moja wa haki za Serikali na umma wa Watanzania kwa ujumla wake na inapaswa kuhakikisha kuwa maslahi ya nchi yanalindwa katika kesi zote za madai ambazo Serikali inashtaki au kushtakiwa ndani na nje ya nchi.

“Ofisi hii inategemewa kuwa itajizatiti kujenga ubobezi kwenye maeneo ya uendeshaji wa kesi za madai na usuluhishi ili kuhakikisha kuwa inashiriki kikamilifu na tena kwa weledi katika kuendesha kesi za madai ndani na nje ya nchi. Kujengwa kwa ubobezi katika ofisi hii, kutalisaidia Taifa kuokoa fedha nyingi ambazo wakati mwingine Serikali hutumia kuwalipa mawakili wa kigeni hususan katika mashauri ya usuluhishi nje ya nchi,” amesema.

Akizungumza kuhusu ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu amesema mabadiliko ya kimuundo yaliyofanywa na Rais Magufuli hayana budi kuwa chachu kwa ofisi hiyo ili iweze kuishauri Serikali katika masuala ya kisheria hususan yale yanayohusu mikataba.

“Kama ilivyo kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nayo inategemewa kuwa itajenga ubobezi katika maeneo mbalimbali ili kuiwezesha kutoa ushauri mzuri kwa Serikali,” ameongeza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema anaunga mkono uamuzi wa Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi wa kutaka kuwepo na kanzidata ya wanasheria wote waliopo nchini ili waweze kutambulika kwa urahisi.

“Pia endeleeni na mpango wa kuwapangua wanasheria kama mlivyojipanga, hii itasaidia kuleta ubobezi kwenye maeneo yao. Pia sheria zibadilishwe na kuwekwa kwenye Kiswahili ili wananchi wazielewe kwa urahisi,” amesema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 15, 2018.


from MPEKUZI

Comments