TRA: Wafanyabiashara Msisubiri Tarehe Za Mwisho Kuomba Msamaha Wa Riba Na Adhabu Ya Kodi

Na Veronica Kazimoto
Wafanyabiashara wenye malimbikizo ya madeni ya kodi wametakiwa kutuma maombi ya msamaha maalumu wa riba na adhabu kwenye malimbikizo hayo mapema kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018 ili waweze kunufaika na msamaha huo ambao umetolewa kwa lengo la kutoa unafuu kwa kuwapa fursa ya kulipa kodi ya msingi  ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19.


Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka wakati wa semina elekezi kwa wafanyabiashara, wadau na washauri wa wafanyabiashara kuhusu msamaha huo iliyofanyika leo mkoani Tabora. 


"Nachukua fursa hii kutoa wito kwenu wafanyabiashara kutuma maombi ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi ambapo mwisho wa kutuma maombi ya msamaha huu ni tarehe 30 Novemba, 2018," alisema Mahendeka. 


Mahendeka aliongeza kuwa "Mara nyingi wafanyabiashara huwa mnajitokeza mwishoni kabisa mwa tarehe zinazoonyesha mwisho wa kulipa, kuwasilisha au kutuma maombi fulani suala linalosababisha foleni na msongamano mkubwa katika kutoa huduma katika ofisi zetu. Nachukua fursa hii kuwaomba msisubiri tarehe za mwisho kuleta barua za maombi ya msamaha huu wa riba na adhabu ya madeni ya kodi na naomba mjue kwamba, huu ndio muda muafaka wa kila mwenye malimbikizo ya madeni kutuma maombi Ofisi ya TRA katika mkoa wake kikodi."


Naye, Afisa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka hiyo Chama Siriwa alisema muombaji wa msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya kodi anapaswa kutoa maelezo na vielelezo vya ukweli na uhakika wakati wa uwasilishaji wa maombi yake.

"Kila muombaji anatakiwa kutoa taarifa za ukweli wakati anaomba msamaha huu na endapo itabainika kuwa muombaji ametoa taarifa za udanganyifu, Kamishna Mkuu anayo haki kisheria kubatilisha na hivyo kupelekea muombaji kupoteza sifa za kufaidika na  msamaha huu, " alifafanua Siriwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mihayo iliyopo mkoani hapa inayomilikiwa na Taasisi ya Dini ya Kanisa Katoliki Padri Salvatory Maganga, ameishukuru TRA kwa kutoa Elimu ya msamaha wa riba na adhabu ya madeni ya malimbikizo ya kodi na kuomba elimu hii iendelee kutolewa kwa wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini.

Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kutoa elimu ya msamaha huu hususani kwa wafanyabiashara, wadau na washauri wa wafanyabiashara kwa lengo la kuwahamasisha kutuma maombi ya msamaha huu kabla ya muda uliopangwa haujamalizika ambao ni tarehe 30 Novemba, mwaka huu. 



Mwisho.
 


from MPEKUZI

Comments