Polisi Wawili Jijini Mwanza Wafukuzwa Kazi

Askari wawili mkoani Mwanza wamefukuzwa kazi baada ya kupatikana na nyara za Serikali ambazo ni meno mawili ya tembo yenye kilo 20.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 28, 2018, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna amesema askari hao, H.5461 Enock wa kikosi cha kutuliza ghasia  mkoa wa Mwanza na H.4165 Robeth wa kikosi maalum walifukuzwa kazi Agosti 27, 2018 kutokana na kosa hilo.

Amesema askari hao walikamatwa Agosti 23, 2018 mtaa wa Nyamhongolo wilayani Ilemela wakiwa na nyara hizo.

Amesema taarifa za awali zilionyesha kuwepo kwa watu wanaojihusisha na biashara ya meno ya tembo, kwa kushirikiana na kikosi kazi cha Taifa cha kupambana na ujangili Kanda ya Ziwa walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Amewataka wote waliokuwa wakishirikiana na askari hao kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi, kwa kuwa wakianza kuwasaka ni lazima watawapata kwa kuwa walifanikiwa kuwamakamata askari hao.


from MPEKUZI

Comments