Mganga Mkuu Wa Serikali Aongoza Timu Ya Wataalam Wa Afya Kukagua Mipaka Ya Nchi Ili Kujikinga Na Ebola.


NA WAMJW
MGANGA Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi ameongoza timu ya wataalam wa Afya kutoka wizara ya afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kukagua na kudhibiti mipaka inayozunguka nchi yetu isipate Ugonjwa wa Ebola.

Akizungumza mara baada ya kukagua mipaka hiyo Prof. Kambi amesema kuwa kwa ujumla ameridhishwa na utayari uliyowekwa na timu za afya za  mkoa hasa  Kigoma na Kagera katika kudhibiti na kujikinga na Ebola.

"Tumekagua mipaka ya Manyovu , Kabanga , Murusagamba , Rusumo na Mutukula na yote tumekuta vitambuzi  na vidhibiti vipo sawa na watumishi wapo tayari kujikinga na kupambana na ugonjwa huu wa Ebola ambao upo nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo" alisema Prof.  Kambi.

Aidha Prof. Kambi amesema kuwa katika kukagua mipaka hiyo pia wanatoa elimu kwa wananchi ma watumishi wa afya ngazi ya mkoa namna ya kutambua , kudhibiti na kujikinga na Ebola endapo ugonjwa huo utaingia nchini.

Mbali na hayo Prof. Kambi amesema kuwa Serikali imeweka nguvu kubwa sana katika kudhibiti na kujikinga na Ebola hasa katika kuhakikisha vifaa vya ukaguzi kama vile Vipima hali joto ( Thermo scanner )vinakua salama kwa matumizi ya mipakani .

Aidha  Prof. Kambi amesema kuwa katika ukaguzi huo walikagua vipima hali joto (Thermo Scanners),  Fomu za kujazia taarifa za  washukiwa wa Ebola na kuwafuatilia wanapokwenda pamoja na kukagua vituo vya muda vya kuhifadhia washukiwa wa ugonjwa huo kabla hawajapelekwa vituo vilivyotengwa na Mkoa husika kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa Prof. Kambi amesema kuwa mpaka sasa kitaalam hakuna aliyebainika kuwa na mgonjwa mwenye dalili za Ebola ambaye amepita mipakani kuja nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Kuhakiki ubora wa huduma za Afya Dkt. Mohammed Ally amesema kuwa  mpaka sasa mipaka iliyohakikiwa imeimarika  na vifaa vya ukaguzi  vinakidhi viwango na ubora katika utambuzi wa washukiwa wa ugonjwa huo.

"Licha ya mipaka kuwa imara kwa hivi sasa lakini tunawaomba timu zote za mipakani kuanzia Uhamiaji, TRA , Jeshi la Polisi na Wahudumu wa Afya kushirikiana kwa pamoja kudhibiti uingiaji holela wa wageni kupitia mipakani ili ugonjwa huo usiingie nchini" alisema Dkt. Mohammed .

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Afya na  Mazingira Dkt.  Khalid Massa amezitaka Halmashauri zote zilizopo katika Mikoa ya Mipakani kuhakikisha wageni wanaolala katika mahoteli kuandika taarifa zao kwa usahihi na kuwafuatilia wateja hao mpaka wanapokwenda ili kudhibiti ugonjwa wa Ebola.

Naye Mtaalam wa kudhibiti Magonjwa ya Mlipuko nchini Tanzania Kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Grace Saguti mesema kuwa Shirika hilo lipo mstari wa mbele katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie kabisa nchini Tanzania.

"Tumeguswa na kinachofanywa na Timu ya Wataalam wa Afya ya Tanzania katika kukagua mipaka yao na ndio mana tumeshirikiana nao katika hili ili kutoa msaada zaidi katika kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini Tanzania" alisema Dkt. Saguti.

Ziara hiyo inayokngozwa na Mganga Mkuu wa Serikali inajumuisha wataalam wa Afya kutoka Wizara ya Afya , WHO na timu za Afya Mikoani imekagua mipaka ya  Manyovu, Musurugamba, Rusumo, Kabanga na Mtukula inayotenganisha Tanzania na nchi za Burundi, Jamhuri ya Watu wa Kongo, Uganda na Rwanda na kumalizia mafunzo kwa timu za Afya za Mikoani kwa ajili ya kidhibiti na kujikinga na Ebola  yanayofanyika mkoani Mwanza.

MWISHO.


from MPEKUZI

Comments