Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma Awaasa Wanasheria Kuzingatia Misingi Ya Taaluma

Na. Idara ya Habari-MAELEZO
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewaasa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma kuzingatia misingi ya taaluma wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mkutano wa pili wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma.

“Mkiwa maafisa wa Mahakama tunawatazamia kufanya kazi zenu kwa kuzingatia misingi ya taaluma iliyowekwa kwa kuzingatia maadili, weledi, uwazi na usiri” alisisitiza he Profesa Juma.

Profesa Juma pia amewakumbusha wanasheria hao walio kwenye utumishi wa umma kuhakikisha  kuwa sheria wanazosimamia zinalenga kuleta ustawi wa wananchi wanyonge na kuiwezesha serikali kutimiza azma yake ya kifanya Tanzania iweze kufikia hadhi ya  nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Vilevile, wanasheria hao wa serikali wameaswa kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutekeleza majukumu yao ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya karne ya 21.

Aliongeza kuwa, wanasheria wanalo jukumu kubwa la kukidhi matarajio ya wananchi ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025,  amani, usalama, umoja, utawala bora, na kujenga uchumi imara.

Kabla ya Jaji Mkuu Profesa Juma, kuhutubia mkutano huo Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palagamba Kabudi  alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya mabadiliko katika muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao unategemewa kuleta ufanisi. Kwenye mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa na Rais Magufuli, yamesababisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali.

Mkutano huo wa siku mbili unawakutanisha wanasheria zaidi ya mia tisa kutoka Wizara, Serikali za mitaa, Mashirika, Wakala na Idara mbalimbali za Serikali.


from MPEKUZI

Comments