CCM Yawatosa Wasanii....Yasema Hakuna Bajeti Yao, Itabaki na TOT

Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally amesema chama hicho hakitakuwa na bajeti kwa ajili ya wasanii na badala yake watabaki na vikundi vilivyopo ndani ya chama.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 31, 2018 wakati akifungua  mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) jijini Dodoma.

Dk Bashiru amesema kwa sasa wasanii watakaoshiriki shughuli za chama hicho, watapewa huduma muhimu pekee ikiwemo malazi, chakula na usafiri.

Akifungua mkutano huo, amesema msanii wa Afrika ni mwana mapinduzi, mpambanaji na kwamba mashairi ya wimbo wake ni lazima yawe na hisia zinazowakera na kuwazomea wanyonyaji.

“Yakowapi mashahiri hayo, ziko wapi nyimbo hizo, ziko wapi ngoma hizo za kusifu bara letu na kuwakumbusha vijana bara hili liliwahi kutawaliwa,” amesema.

“Ndio maana nimesema ndani ya CCM hatutakuwa na bajeti ya wasanii tena, hakuna tutabaki na TOT tutaimarisha chombo chetu kile kama alama na Vijana Jazz basi. Tukienda Arusha tutawakuta wasanii kule wataimba mashairi, watacheza ngoma.”

Amesema alipopokelewa makao makuu ya chama hicho aliburudishwa na vikundi vya ngoma, kubainisha kuwa si kwamba wasanii wa nyimbo alizoziita za kurukaruka ni wabaya, bali kibaya kwa mtazamo wake ni ujumbe uliomo ndani ya sanaa hiyo.


from MPEKUZI

Comments