Benki Ya Standard Charted Kuimwagia Tanzania Sh. Trilioni 3.3 Kujenga Reli Ya Kisasa-SGR

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
BENKI ya Standard Chartered Group imekubali kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.46 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 3.3 kwa ajili ya kujenga kipande cha Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kuanzia Morogoro hadi Makutupora, mkoani Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Bill Winters, Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mpango ameishukuru Benki hiyo kwa kukubali kugharamia ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa ambayo lengo lake ni kuimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwenda bara na nchi jirani za Maziwa Makuu na zile ambazo hazipakani na Bahari.

"Tunajenga Reli hiyo ya Kisasa kutoka Dar es Salaam - Morogoro hadi Makutupora ambazo ni awamu mbili lakini pia tutajenga reli hiyo kuelekea Isaka mpaka Mwanza na baadaye Rusumo ambapo wenzetu wa nchi ya Rwanda, tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi Kigali" Aliongeza Dkt. Mpango

Aidha, Dkt. Mpango amemweleza Kiongozi huyo wa Juu kabisa wa Benki ya Standard Chartered Group anayeongoza Benki hiyo kwenye nchi zaidi ya 60 duniani, kuhusu vipaumbele vikubwa vya nchi ikiwemo kuboresha Shirika la Ndege la Taifa-ATCL, na Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Mto Rufiji.

"Tunaimarisha Shirika letu la Ndege ili kuimarisha sekta ya utalii kwa sababu tuna vivutio vingi na haipendezi wageni wanao kuja nchini wanafikia nchi jirani, sasa ifike wakati tuwe na uwezo wa kuwasafirisha moja kwa moja kuja nchini kwetu" Alisisitiza Dkt. Mpango.

Alisema Tanzania ni ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikitanguliwa na Brazil lakini inapokea watalii wasiozidi milioni 2 kwa mwaka jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka ili sekta hiyo ichangie uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa kupitia fedha za kigeni.

Alisema katika kulifufua Shirika hilo la Ndege, tayari Serikali imenunua ndege nne ikiwemo ndege kubwa aina ya Boeing 787- 8 Dreamliner na kwamba ndege nyingine 3 zitakuwa zimewasili nchini ifikapo mwezi Juni, mwakani, na kulifanya shirika hilo kuwa na ndege 7. 

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji na kuendeleza ujuzi kwa wananchi ili waweze kufanyakazi kwenye viwanda na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa ujumla kwa kuwa maendeleo yanahusu watu.

Akizungumza kwenye mkutano wake na Dkt. Mpango, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Group, Bw. Bill Winters, ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na kwamba Benki yake itatoa mkopo huo na kuahidi kuwa balozi wa kuelezea mafanikio makubwa ya kiuchumi ya Tanzania kwa wadau wengine.

Aliahidi kuzishawishi taasisi nyingine za fedha ulimwenguni kuangalia uwezekano wa kuunga mkono jitihada hizo ambazo mwisho wake wanufaika wakubwa watakuwa ni wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.

"Tunaimani kubwa na uwezo wa Tanzania pamoja na fursa nyingi za kiuchumi ilizonazo na kwamba miradi mingi ya kipaumbele iliyoainishwa itafikiwa na tunalo jukumu kama Benki kutoa fedha na kuiweka miradi hiyo pia sokoni ili iweze kupata fedha" Alisisitiza Bw. Bill Winters.

Katika kikao hicho, Bw. Bill Winters aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Kenya na nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Lamin Manjang na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Tanzania Bw. Sanjay Rughani, ambapo pia Benki hiyo inafanya shughuli zake hapa nchini kwa kipindi cha miaka 101 sasa.

Mwisho


from MPEKUZI

Comments