Waziri Mkuu: Fuatilieni Madai ya Wakulima wa Kahawa

WAZIRI Mkuu Kasimu Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri wa Kilimo, Bw. Omary Mgumba afuatilie sh. milioni 150 walizotakiwa kulipwa wakulima wa kahawa wa chama cha msingi cha  Kalinzi Organic Coffee Grower   zilizolipwa kwenye kikundi kingine.

Ametoa maagizo hayo jana (Jumatatu, Julai 30, 2018) wakati alipotembelea shamba la kahawa katika kata ya Nyarubanda  Wilayani Kigoma, akiwa njiani kuelekea wilaya ya Buhigwe kwa ajili ya kuendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.

Ametoa metoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba kumuomba awasaidie kutatua changamoto ya malipo ya wakulima wa chama Kalinzi Organic Coffee Grower ambayo hayajalipwa baada ya kuuza kahawa yao katika chama cha kahawa moshi miaka saba iliyopita.

Waziri Mkuu amesema  wakulima  hao wanatakiwa kulipwa fedha zao kwa wakati, hivyo amemuagiza Waziri Mgumba kuhakikisha anafuatilia ni kwanini fedha hizo zililipwa kwa wakulima wa kikundi kingine. Pia ahakikishe wakulima hao wanapata haki yao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaomba wakaulima hao kupanda miche mipya na kuachana na ya zamani kwa kuwa uzalishaji wake ni mdogo na inashambuliwa sana na magonjwa ukilinganisha na miche ya kisasa.

Aidha, Naibu Waziri huyo wa Kilimo Omary Mgumba alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na ni kweli kuwa fedha hizo zililipwa kimakosa na Bodi ya Kahawa kwenda kwa chama cha Msingi cha Kalinzi Farm Coffee badala ya chama cha Kalinzi Organic Coffee Grower.  Ameahidi kufuatilia suala hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kalinzi Organic Coffee Grower , Bw. Said Mchachu alisema chama chao kina wakulima 447 ambao tangu wapeleke kahawa yao Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuiuza mwaka 2012 mpaka sasa wanaendelea kufuatilia madai yao bila mafanikio.

Alisema madai hayo yamesababisha migogoro ndani ya chama chao kufuatia baadhi ya wakulima wakiwatuhumu viongozi kuwa wao ndio wamekula fedha zao jambo ambalo si kweli, hivyo alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia ili waweze kupata fedha zao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI

Comments