Wachimbaji Wadogo Watakiwa Kulipa Maduhuli Ya Serikali

Na Jonas Kamaleki-MAELEZO, Dodoma
Serikali imewataka wachimbaji wadogo wadogo Mkoani Dodoma kulipa maduhuli yake ili kuiwezesha kutekeleza mipango yake ya maendeleo ikiwemo kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji hao.

Rai hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji madini Mkoani Dodoma.

“Utakuta leseni moja inatumiwa na watu kama kumi ambao hawalipi kodi ya Serikali, hii haivumiliki, ulipaji wa maduhuli hayo uanze mara moja”, alisema Prof. Kikula.

Akiongea kuhusu uchenjuaji wa dhahabu baada ya kutembela kiwanda hicho, Prof. Kikula amesema kuwa kuna changamoto katika uchenjuaji, hivyo imeundwa timu ndogo ya kufuzifuatilia ili utatuzi wake uweze kupatikana.

Changamoto zilizobainishwa na wachenjuaji ni pamoja na kutokuwa na umeme wa uhakika katika viwanda vyao, hivyo kuiomba Serikali kuingilia kati.

Naye Meneja wa Mgodi wa Nholi, Raphael Simba ameishukuru Serikali kwa kufanya ziara mgodini hapo kwani itawasaidia kutatua changamoto wanazokumbana nazo.

Simba amebainisha changamoto wanazokutana nazo kuwa ni uchimbaji wa kizamani unaotumia zana zisizoridhisha.

Ameiomba Serikali kuwasaidia katika upatikanaji wa zana za kisasa ikiwemo na umeme, kuwapatia wataalaam wa miamba kwa ajili ya kuainisha maeneo yenye dhahabu, jambo ambalo litawapunguzia kutumia nguvu nyingi katika kuchimba sehemu zisizo na madini hayo.

Aidha, Simba ameiomba Serikali kuwapatia mafunzo ya uchimbaji bora na wenye tija ikiwemo kuwafundisha kuhusu Sheria ya Madini ya Mwaka 2017. Akijibu kuhusu mafunzo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini amemwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa kwa kushirikiana na Kamishina wa Tume, Haroun Kinega kutoa mafunzo hayo kuanzia wiki ijayo.

Kwa upande wake, Kamishina wa Tume ya Madini ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Madini nchini, Haroun Kinega amesema katika ziara hiyo, amebaini changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wadogo na kwamba zitafanyiwa kazi ili uchimbaji uwe na tija kwa wachimbaji na Serikali iweze kupata mapato yake.

Amesisitiza kuwa Tume itaendelea kukagua shughuli za uchimbaji na kuwapa elimu hasa wachimbaji wadogo wadogo kwa ajili ya kuboresha uchimbaji huo hivyo kuwaongezea kipato.

Ziara hiyo inayolenga kuainisha changamoto za uchimbaji madini na kuzitafutia suluhisho itaendelea wiki ijayo katika Mkoa wa Dodoma.


from MPEKUZI

Comments