Serikali Yasema Haina Taarifa ya Gazeti la Mwanahalisi Kushinda Kesi Mahakamani

Wakati mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya HaliHalisi, Saed Kubenea amesema Jumatano ijayo atachapisha nakala ya kwanza ya gazeti la Mwanahalisi baada ya kushinda kesi katika Mahakama Kuu, Serikali imesema haina taarifa na ujio huo.

Kubenea aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba, gazeti hilo limeshinda kesi iliyofunguliwa mwaka 2017 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na uamuzi umefanyika hukumu ilitolewa Jumanne ya wiki iliyopita.

“Kama kampuni Jumatano ya wiki ijayo, tutachapisha nakala ya gazeti hilo kwa mara ya kwanza tangu lifungiwe,” alisema.

Alisema taratibu za kuomba leseni zinaendelea lakini gazeti kwa mujibu wa sheria halihitaji kusajiliwa tena badala yake, Mahakama imeamuru lifunguliwe na liendelee kuchapishwa.

Kubenea ambaye pia ni mbunge wa Ubungo (Chadema), alisema Mahakama imesema mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) hana mamlaka yoyote siyo tu kuomba watoe maelezo ni kwa nini walichapisha habari hiyo, bali hata kuwaomba wapeleke utetezi wao.

Hata hivyo, mkurugenzi wa Maelezo ambaye pia ni msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alisema wao kama Serikali hawana taarifa ya hukumu hiyo.

Alisema mbali na kutokuwa na taarifa ya kushinda kesi hiyo, kuna taratibu chini ya sheria ya huduma za habari zinazotakiwa kufuatwa kabla gazeti halijachapishwa.

 “Sheria hiyo imeanza kutumika Desemba 31 mwaka 2016 ambayo inaeleza kwa namna yoyote ile hakuna gazeti litakaloruhusiwa kuchapishwa bila kuwa na leseni period (basi), ”alisema Dk Abbas.

Kubenea alisema wananchi waendelee kuuamini mhimili wa mahakama, wasiache kudai haki zao mahakamani, kuweka mawakili wazuri na kuwasilisha ushahidi usio na shaka kwa sababu mahakama zipo huru.

Awali, mwanasheria wa kampuni hiyo, Nashon Nkungu alisema Mahakama imesema amri ya kulifungia gazeti hilo ni batili na haikufuata taratibu za sheria ikiwamo kutokuwa na haki ya usikilizwaji kwa upande wa mlalamikaji.

Pia, alisema Mahakama ilieleza kuwa mkurugenzi wa maelezo hakuwa na mamlaka ya kutoa amri hiyo wala kuchukua uamuzi hayo.


from MPEKUZI

Comments