Lugola Amtaka Zitto Kabwe Ajisalimishe Polisi Haraka Sana

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amemtaka mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kujisalimisha kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi kwa maelezo kuwa ametoa kauli za uchochezi.

Lugola ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 31, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Amesema Zitto ametoa kauli za uchochezi na kuwatukana viongozi wa Serikali wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Kilwa Kusini.

Katika mkutano huo Zitto alialikwa na mbunge wa jimbo hilo, Seleman Bungara maarufu Bwege.

“Kosa jingine la Zitto ni kwenda kufanya mkutano eneo ambalo sio la kwake kwa mujibu wa taratibu. Nampa siku mbili ajisalimishe kwa RPC (Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi),” amesema Lugola.

“Akikaidi nitamuagiza IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini-Simon Sirro) amkamate popote alipo. Nilishasema na nitaendelea kusema katika uchaguzi huu na zijazo watu wanaotukana  viongozi hawatabaki salama.”


from MPEKUZI

Comments