Familia Yakubali kumzika Ndugu yao aliyekufa mikononi mwa polisi

Ndugu wa Pascal Kanyembe (39) aliyefariki dunia akiwa chini ya ulinzi wa polisi wamekubali kuzika mwili wa mkazi huyo wa kijiji cha Rubambagwe wilayani Chato  baada ya kususia kwa siku nne.

Kanyembe alikamatwa na polisi saa 7:00 usiku wa Julai 23, 2018 na  kufariki dunia mikononi wa askari wa doria muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya wilaya kwa matibabu.

Ndugu hao walisusa kuzika mwili wa ndugu yao, wakitaka kuelezwa sababu za kifo chake kwa kuwa mwili wake ulikuwa na majeraha miguuni, bega la kushoto, usoni na upande wa kushoto kichwani.

Mkuu wa wilaya ya Chato, Shaban Ntarambe  jana alisema wamefanya kikao na familia ya marehemu, wamekubaliana kuzika na Serikali itatoa jeneza.

Alisema kutokana na kifo hicho kuwa na utata  Julai 26, 2018 walikutana na familia na kufanya kikao bila kufikia muafaka na hivyo  kulazimika kufanya kikao kingine jana .

Alisema ndugu hao walikataa kuzika kwa sababu walitaka kujua nani aliyesababisha kifo cha ndugu yao.

“Tumekubali kushirikiana na ndugu na tutatoa jeneza. Muhimu ni kumhifadhi marehemu, tumewaeleza wazi kuwa kifo hakina fidia na hata wakitaka fidia ndugu yao hawezi kurudi na Serikali haijamtuma mtu kuua,” alisema.

Kanyembe atazikwa leo wilayani humo.


from MPEKUZI

Comments