Tanzania Yaongoza Kwa Wanyama Pori Afrika......Ni baada ya Serikali na wananchi kulinda rasilimali za nchi

IMEELEZWA kuwa jitihada za Serikali za kulinda rasilimali za nchi na ushirikiano kutoka kwa wananchi zimesababisha ongezeko kubwa la idadi ya wanyama pori, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye wanyama wengi barani Afrika.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) katika hotuba yake aliyoitoa bungeni wakati wakuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma.

Amesema ili kuitumia vema fursa ya kuwa na vivutio vingi ikiwemo wanyamapori wengi na kuleta tija kwa nchi, Serikali imeendelea kuandaa utambulisho wa Tanzania Kimataifa (Destination Branding), lengo likiwa ni kuitambulisha Tanzania kama kituo mahsusi cha utalii duniani.

“Tunalenga kuvutia wageni wa kimataifa waje kuitembelea Tanzania, kuongeza wigo wa kutangaza vivutio na kufanya vivutio vya utalii vifahamike duniani. Pia, Serikali inakamilisha mchakato wa kuanzisha Channelmaalum katika Television ya Taifa (TBC1) kwa ajili ya kutangaza utalii,” amesema.

Waziri Mkuu amesema maandalizi ya kuanzisha studio ya kutangaza utalii kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaendelea vizuri, ambapo studio hiyo itawezesha kutambua, kufuatilia na kuwasiliana moja kwa moja na watu wanaofuatilia Tanzania na vivutio vyake.

Pia, Serikali inakusudia kuanzisha chombo kitakacho simamia fukwe za bahari, mito na maziwa lengo la hatua hiyo ni kuimarisha utalii wa fukwe Bara na Visiwani kwa kujenga hoteli, maeneo ya mapumziko na michezo mbalimbali.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto ya migogoro ya matumizi ya ardhi miongoni mwa watumiaji kwa kuunda timu ya kisekta ikijumuisha watendaji wa sekta mbalimbali zinazohusika kwenye masuala hayo.

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kupima mipaka ya vijiji, kutunga na kurekebisha sera, sheria na kuandaa mipango mbalimbali ya kuboresha matumizi na utawala wa ardhi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa mipango ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini. “Ni matumaini yangu kwamba programu hii ikitekelezwa, ardhi itatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii na pia kudhibiti migogoro ya ardhi,”.

Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2018/19, Serikali itaendelea kutatua migogoro inayojitokeza na pia kutoa elimu kwa umma ili watumiaji wote wa ardhi waweze kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa katika vijiji.

Amesema katika juhudi za kudhibiti migogoro kwenye maeneo mbalimbali ya utawala, jumla ya vijiji 11,256 kati ya vijiji 12,545 vilivyopo nchini vimepimwa, hiyo ni sawa na asilimia 90 ya vijiji vyote, huku lengo likiwa ni kupima mipaka ya vijiji vyote na kuvipatia vyeti vya kijiji kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

“Hatua hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji. Ili kuharakisha kasi ya upimaji nchini, Serikali itaendelea kutumia makampuni binafsi ya upimaji na upangaji makazi kwa vibali maalum,”.

Akizungumzia kuhusu hifadhi ya mazingira, Waziri Mkuu amesema misitu inaendelea kukatwa hovyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya mkaa na kuni, ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kote nchini.

Amesema Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu mahsusi wa kuwawezesha na kuwaratibu wajasiramali wanaojishughulisha na nishati mbadala ili kuwa na uzalishaji wa kutosha wa nishati hiyo na iweze kusambazwa katika maeneo yote nchini.

Aidha, Serikali itaendelea kuboresha na kukamilisha Mkakati wa Tungamotaka (National Biomass Energy Strategy) na kusambaza kwa wadau nchini ili kuratibu vyema upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo.


from MPEKUZI

Comments