Mwanasheria Mkuu wa Serikali Awajibu Wabunge Waliotaka Ahojiwe na Kamati ya Maadili kwa Kulipotosha Bunge

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi amewajibu wabunge waliotaka ahojiwe na Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa madai ya kukidanganya chombo hicho cha Dola kuwa fedha za ushuru wa mauzo ya korosho nje ni za umma.

Wabunge waliomuomba Spika Job Ndugai kuitaka kamati hiyo kumhoji na kumchukulia hatua AG ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini) na Cecil Mwambe (Ndanda).

Akiwajibu wabunge hao AG amesema si kweli kuwa ushuru huo ulianzishwa na Serikali si wakulima, kwamba Bodi ya Korosho ilikuwa ikikusanya kwa niaba ya Serikali.

“Tozo hii haikuanzishwa na wakulima. Bodi ya korosho ilianzishwa kwa sheria ya mwaka 1984 . Lakini mwaka  1998 kulitokea ubadhilifu fedha, Serikali ilitoa maelezo kuwa fedha zisipelekwe mfuko wa Korosho,”amesema.

Amesema  mfuko huo haukuridhika na maelekezo ya Serikali na hivyo ikafungua kesi Mahakama Kuu na kutoa uamuzi kuwa bodi ya korosho inakusanya fedha za Serikali na Serikali ina mamlaka na fedha hizo.

“Mfuko haukuridhika, ukakata rufaa lakini mahakama ya rufaa ilitupilia mbali rufaa hiyo hivyo kisheria uamuzi wa mahakama kuu unabaki ule ule (kwamba fedha hizo ni za umma),”amesema kilangi.

Kuhusu kauli ya kwamba wakulima wa korosho waliingia mkataba na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kukusanya kodi, mwanasheria huyo amesema hakuna mtu anayeweza kupatana na TRA kukusanya kodi.

“Hatuna mtu yoyote anaweza kukusanyiwa kodi na TRA. Huu ni upotoshaji. Marekebisho ya Sheria ya Korosho ya mwaka 2009 hayatambui mfuko wa kuendeleza korosho.  Haiwezekani kuutambua mfuko kisheria,”amesema.

Amesema kwa mujibu wa Katiba na sheria za fedha, TRA ikishakusanya fedha inatakiwa kupeleka katika mfuko mkuu wa Serikali, hivyo kufanya vingine ni kuvunja Katiba na Sheria.

Kuhusu kufuta Tume ya Mpango, Dk Kilangi amesema kufuta tume hiyo hakuna shida kwasababu majukumu yake yatahamishiwa kwenye wizara na kwamba sheria inaweza kutungwa upya kwasababu hakuna shida katika hilo.


from MPEKUZI

Comments