Magazeti Yanayoandika Habari za Uchochezi wa Kidini, Kikabila Kushitakiwa

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema wanaochukizwa na magazeti yanayoandika kuhusu ukabila na udini waende mahakamani na wizara itakuwa shahidi namba moja.

Akijibu hoja zilizojitokeza bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 ya Sh32.45 trilioni leo Juni 26, 2018 amesema jana kulijitokeza suala la ukabila ambalo haliwezi kubaki katika taarifa rasmi za Bunge bila kujibiwa.

Dk Mwakyembe amesema suala hilo lilizungumzwa na mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia.

“Mbunge ninayemuheshimu sana na mdogo wangu Mbatia, pamoja na maudhi yote tunayoweza kuyapata, sisi viongozi tusikubali kwa njia yoyote kuwa katika basi la ukabila na udini na tukifanya hivyo tutasahau mafanikio makubwa tuliyoyapata hasa kujenga umoja,” amesema Dk Mwakyembe.

Amesema mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aligusia magazeti ya Tanzanite na Jamvi la Habari, kwamba yana ubaguzi wa Wachanga.

“Haya magazeti yanaweza kushitakiwa na sheria ya habari kifungu cha 41 na unaweza kuyapeleka mahakamani,” amesema waziri Mwakyembe.

Amesema, “Kama umetukanwa wewe nenda mahakamani na sisi tukakuwa shahidi. Hivi leo Mchaga ni nani, nani anaweza kushika jiwe na asimguse mkewe au mjomba wake.”

Waziri Mwakyembe amesema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipigania uhuru wa nchi na wenye kuwaweka Watanzania katika umoja bila ukabila na udini.

Amesisitiza wananchi kudumisha amani na umoja na kuepuka ukabila na udini.

Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza baada ya majibu ya Dk Mwakyembe amesema, “Hili jambo la ukabila si la kuliendekeza kusema hapa, tunaweza kusema tunadhani tunajenga kumbe tunafanya makosa makubwa.”

Ndugai amesema, “Unaweza kujikuta unalalamika jambo fulani kumbe jamii hiyo iko serikalini na kama kuna shida katika jambo hilo, tunong’one pembeni.”

Spika Ndugai amesema, “Makundi ya kisiasa na kijamii, tuendelee kuwa Watanzania wamoja na dalili za ukabila ni mbaya. Hatuwezi kufika popote kama tunaendekeza ukabila.”


from MPEKUZI

Comments