Hatima ya Mbowe na wenzake kujulikana Julai 2

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, July 2,2018 inatarajia kutoa uamuzi wa muda wa kusitisha ama kutositisha usikilizaji wa kesi inayowakabili viongozi wa CHADEMA akiwemo mwenyekiti wake Freeman Mbowe.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kupinga maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi amewasilisha maombi hati kinzani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri ambapo amepinga usitishwaji wa kesi hiyo kwa sababu maombi yao ni batili.

Kadushi amedai msingi mkuu wa pingamizi hizo ni kwamba maombi ya waombaji ni batili kwa kuwa utaratibu uliotumika kuielekeza mahakama hiyo iweze kutoa amri walizoomba una dosari.

Amedai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo na kutoa nafuu zilizoombwa, hivyo aliomba yatupiliwe mbali.

Katika maombi ya upande wa utetezi, yaliyowasiishwa na Peter Kibatala wameiomba mahakama isimamishe kwa muda usikilizwaji wa kesi hiyo kwa sababu wamewasilisha maombi ya marejeo Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya uamuzi mdogo uliotolewa na mahakama hiyo.

Kutokana na mvutano wa kisheria, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi July 2,2018.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Pia wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko.

Inadaiwa kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo February 16, mwaka huu katika maeneo ya Viwanja vya Buibui, Mwananyamala na barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni.

Wanadaiwa kuwa February 16,mwaka huu katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washitakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani.

Inadaiwa kitendo cha kugoma kulisababisha hofu iliyochangia kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.


from MPEKUZI

Comments