Tume ya Madini Kutekeleza Majukumu Yake Kwa Maslahi Ya Taifa

Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma
Tume ya Madini imetakiwa  kuhakikisha inatekeleza kikamilifu jukumu la usimamizi, Udhibiti, Ukaguzi, Ufuatiliaji, Ukusanyaji wa taarifa na kuweka kumbukumbu kwa kusimamia sekta hiyo kwa uadilifu  hali itakayosaidia Taifa kunufaika na uwepo wa rasilimali madini.

Akizungumza wakati akizindua Tume hiyo Jijini Dodoma, Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa kuzinduliwa kwa Tume hiyo  kunaashiria kuanza kwa ukurasa mpya katika sekta ya madini nchini kwa kuwa uamuzi huo ni mapinduzi makubwa hali itakayosaidia wananchi  kunufaika na sekta hiyo.

“Ni imani yangu, na pia ni imani ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na imani ya Watanzania wote kuwa mtatubadilishia simulizi za sekta ya madini kutoka kuwa za kukatisha tamaa na kuwa za matumaini, kuibadili historia ya sekta ya madini kutoka kuwa ya miguno na manunguniko na kuwa yakujivunia” Alisisitiza Mhe. Kairuki

Akifafanua Mhe. Kairuki amesema kuwa, si kwamba Tume hiyo imepewa mamlaka makubwa bali pia imepewa imani kubwa kwa kuwa mamlaka makubwa yanakuja na wajibu mkubwa mikononi mwa watendaji wa Tume hiyo.

Aliongeza kuwa Watanzania wana matarajio makubwa na Tume hiyo na viongozi wake kwa kuwa Serikali na wananchi wanaamini kuwa sekta hiyo sasa iko katika mikono  safi na salama.

Kutokana na imani hiyo Mhe. Kairuki amesema kuwa  wananchi wanaamini Tume hiyo itatenda haki, kusimamia ukweli na kuzingatia maslahi ya kizazi hiki na kijacho ili viweze kunufaika na  madini ambayo Mwenyezi Mungu amelijalia Taifa letu.

Aidha, Mhe. Kairuki ameitaka Tume hiyo kuhakikisha inasimia kikamilifu wachimbaji wadogo  kwa kuwatambua na kurasimisha shughuli zao ili sekta hiyo iwanufaishe kama ilivyo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa upande wa vibali vya mauzo ya madini nje ya Nchi amesema kuwa ni vyema  Tume ikafanya mapitio ya fomu na vibali ili kuhakikisha kuna maelezo na taarifa za kina za madini yanayosafirishwa kuhusu yalipotoka (origin),.

Vile vile kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama  ameitaka Tume iandae mbinu na mikakati ya kudhibiti utoroshaji wa madini ili kudhibiti biashara haramu ya madini.

Tume ya madini imetakiwa kuangalia uwezekano wa kuweka utaratibu wa kutoa bei elekezi za madini ya aina mbalimbali ambapo utaratibu huo utawasaidia wachimbaji wadogo na wa kati.

Pia  Mhe. Kairuki  ameitaka Tume hiyo kuhakikisha kuwa kila anayefanya biashara ya madini ana leseni na ni leseni hai iliyolipiwa na kuhakikisha kwamba inathibiti watu  au makampuni yanayomiliki leseni walizopewa kwa muda mrefu bila kuziendeleza kinyume na masharti ya leseni hizo.

Kuwepo kwa utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuona maendeleo ya  uwekezaji katika migodi ambayo imepata leseni ni moja ya jukumu ambalo Tume hiyo inatakiwa kulitekeleza.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idrissa  Kikula amesema kuwa wamepokea maelekezo yote ya Serikali na Tume hiyo iko tayari kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa .

Aliongeza kuwa Tume imejipanga kuhakikisha kuwa inatatua migogoro iliyopo katika sekta hiyo kwa kushirikisha vyama vyao vilivyopo katika maeneo yao.

Tume ya Madini imeundwa ikiwa ni sehemu ya  juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa rasilimali za Taifa zinawanufaisha wananchi wote,  Kutokana na azma hiyo Tume imepewa jukumu la kusimamia sekta ya madini na Wizara ya Madini kubaki na Masuala ya kisera.


from MPEKUZI

Comments