Wizara Ya Afya Yazindua Mfumo Wa Tehama Kwa Vituo Vya Kutolea Huduma Za Afya Nchini

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Wizara wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  imezindua mfumo mpya wa TEHAMA kwa vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa na lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya katika  vituo vyote hapa nchini.

Uzinduzi huo umefanywa na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo, Jijini Dodoma ambapo pia alizindua kanuni za sheria ya uongozi wa hospitali za watu binafsi, mwongozo wa viwango vya msingi kwa vituo vya kutolea huduma za afya nchini pamoja uzinduzi wa bodi mpya ya ushauri wa hospitali za watu binafsi.

“Nina uhakika maombi ya usajili wa vituo vya afya sasa yataenda kwa haraka. Waombaji watajaza fomu na kulipia hukohuko walipo bila kufika ofisini  na vile vile watakuwa na uwezo wa kutumia mfumo kwa kutumia simu zao,” alisema Dkt. Ndugulile.

Amesema Sekta ya Afya ni miongoni mwa sekta muhimu katika Serikali ya Awamu ya Tano ambapo sekta hiyo ni ya tatu kwa kupata  bajeti kubwa. Aidha  kwa mwaka huu wa  fedha jumla ya vituo vya afya 208 vimeboreshwa kwa ajili ya kutoa huduma ya dharura ya mama na mtoto.

Dkt. Ndugulile amesema ndani ya bajeti hii vituo vya afya 67 vitajengwa nchini pamoja na hospitali za rufaa kwa mikoa ambayo haina hospitali za rufaa.

Wakati huo huo, Waziri Ndugulile ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima wa Afya (NHIF) kufanya majukumu iliyopewa ikiwa ni pamoja kusajili vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma kutokana na vigezo vilivyowekwa na mfuko huo na kuziachia mamlaka  nyingine majukumu yake ya kukagua vituo hivyo kama vile mikataba ya kazi ya wafanyakazi wa vituo husika.

Aidha ameutaka mfuko huo kutafakari juu ya masharti yaliyowekwa katika kusajili vituo ambapo kituo hakiwezi kusajiliwa mpaka kiwe katika uangalizi na mfuko huo kwa miaka isiyopungua mitano.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Otilia Gowele amesema kanuni mpya za sheria ya uongozi wa hospitali za watu binafsi zitasaidia kusogeza huduma kwa wananchi pia hospitali hizo kutoa huduma kulingana na mahitaji ya sasa.


from MPEKUZI

Comments