Kikwete afunguka kuuwawa mdogo wa Heche na polisi

Mbunge wa jimbo la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mh. Ridhiwani Kikwete amefunguka na kusema kitendo cha polisi mwenye namba E1156 Koplo William Marwa ambaye anadaiwa kufanya mauaji kwa mdogo wa Heche kimemsikitisha sana.

Ridhiwani amefunguka hayo baada ya Jeshi la Polisi kanda Maalum ya Tarime na Rorya kudai kuwa linamshikilia polisi huyo kwa tuhuma za kumchoma kisu Bwana Chacha Heche Suguta ambaye ni mdogo wa Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche.

"Kitendo kilichotokea sio tu kimesikitisha ukoo wa Bwana Heche lakini kwangu binafsi. Jeshi letu limetengenezwa kulinda watu na mali zao sio kuumiza wasio na hatia. Ni imani yangu Serikali itasimamia haki kwa familia ya Heche. Poleni sana kwa msiba. Mungu awape subira John Heche" alisema Ridhiwani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya, Henry Mwaibambe amethibitisha kumshikilia askari wake mwenye namba E1156 Koplo William Marwa kwa tuhuma za kusababisha kifo cha kijana Saguta Chacha mwenye umri wa miaka 26 mkazi wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara kwa kumchoma Kisu.


from MPEKUZI

Comments