Kamati ya Bunge yaipinga serikali kuhamisha walimu

Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imekosoa utaratibu wa Serikali kuhamisha baadhi ya walimu wa shule za sekondari kufundisha shule za msingi kwa maelezo kuwa kila ngazi ya ualimu ina miongozo na mafunzo yake mahsusi.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2018/19 kwa niaba ya mwenyekiti, Peter Serukamba, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema Serikali inatakiwa kuliangalia suala hilo kwa jicho la pekee.

“Kamati inatambua na kuelewa tatizo la ukosefu wa walimu hasa katika shule za msingi hapa nchini, ila kuchukua walimu wa sekondari kwenda kufundisha shule za msingi si sawa,” amesema Bashe.

Mbunge huyo ameyasema hayo leo Aprili 30 bungeni mjini Dodoma.

“Kumchukua mwalimu wa sekondari kwenda kufundisha shule ya msingi kumepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa jamii na walimu wenyewe ikiwemo kuhisi kuadhibiwa hivyo kushusha morali ya kufanya kazi.”

Amesema Serikali inapaswa kutazama uamuzi huo kwa jicho la pekee na kufanya uamuzi ulio sahihi kwa mustakabali mzuri wa elimu nchini.

Pia, amesema kamati hiyo ina taarifa kuwa mahitaji ya walimu kwa shule za msingi ni 273,454 lakini walimu waliopo ni 175,946 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 97,508 sawa na asilimia 35.

“Kwa shule za sekondari hasa masomo ya sayansi, mahitaji ni walimu 35,136 lakini waliopo ni 19,285 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 15,851 sawa na asilimia 45.1,” amesema Bashe.


from MPEKUZI

Comments