CHADEMA wakanusha habari ya Tundu Lissu kuwasili muda wowote

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kimekanusha taarifa zinazoendelea mitandaoni kuhusu uwezekano wa kurejea nchini kwa Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu kutokea Ubelgiji alipokuwa akipatiwa matibabu tangu mapema Januari mwaka huu.

Kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano CHADEMA, Ndg. Tumaini Makene amesema kwamba kupitia mitandaoni mapema leo kumekuwa na taarifa za kwamba Lissu anatarajiwa kurejea nyumbani Tanzania wakati wowote kuanzia juzi, kwamba amemaliza matibabu yake kitu ambacho sicho cha kweli na kimezua taharuki.

Katika taarifa yake Ndg. Makene amesema kwamba Mwanasheria huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, hajazungumza na mwandishi wa habari yeyote juu ya kurejea kwake nyumbani kwa sababu zilizo wazi kabisa kuwa bado hajapona na anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mwingine mwisho wiki hii au wiki ijayo.

Hata hivyo chama hicho kimetoa wito kwa na wanachama na Watanzania wote wenye mapenzi mema kutokana na kuguswa na uzito wa masahibu yaliyompata Lissu wameendelea kuguswa na kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya matibabu na hali ya afya yake kupuuza taarifa hizo.

Tundu Lissu yupo nchini Ubelgiji akipatiwa awamu ya tatu ya matibabu baada ya kumaliza matibabu nchini Kenya mwezi Januari ambapo alikuwepo huko kwa takribani miezi minne ambapo alikuwa akiuguza majeraha ya risasi.

Mbunge huyo machachari alipigwa risasi zilizokadiriwa 37 nje ya makazi yake huko Jijini Dodoma majira ya saa 7 mchana na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akitoka kwenye majukumu yake ya kibunge.


from MPEKUZI

Comments