Serikali Kuweka Alama za Kimataifa Mipaka ya Kenya na Uganda

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema serikali itaanza kuweka alama za mipaka ya kimataifa katika mipaka yake na nchi jirani za Kenya na Uganda kuanzia mwezi ujao.

Hatua hiyo inatokana na baadhi ya alama za mipaka yake na nchi jirani katika maeneo mbalimbali kuharibika ama kuchezewa na hivyo kuleta mkanganyiko na nchi hizo.

Akizungumza katika ziara yake mkoani Mara mwishoni mwa wiki, Mabula alisema kwa sasa fedha kwa ajili ya kazi hiyo imeshatengwa na kinachosubiriwa ni kuanza rasmi kwa kazi hiyo mwezi ujao.

"Katika zoezi la kuweka alama za mipaka vitawekwa vigingi kila baada ya umbali wa mita mia moja sambamba na kubainishwa eneo la ardhi huru," alisema Mabula.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa serikali, tayari timu ya wataalamu kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania zimeshakutana na kukubaliana kuhusiana na uainishaji mipaka ya nchi hizo.

Mabula alisema kwa kuanzia alama zitawekwa katika mipaka iliyopo mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga na baadaye zoezi litaendelea katika maeneo mengine ya mipaka ya nchi.

Alisema ni imani yake kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la kuweka alama za kimataifa za mipaka, migogoro kuhusiana na mipaka itakwisha.

Mara ya mwisho Tanzania kuweka alama za mipaka ya kimataifa kati yake na nchi jirani ilikuwa mwaka 1975, ikiwa ni utekelezaji wa Tangazo la Serikali (GN) mwaka 1965 kuhusiana na mipaka.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Grorious Luoga, alimweleza naibu waziri huyo kuwa, mbali na suala la mipaka ya kimataifa, wilaya yake inakabiliwa na changamoto ya mipaka baina ya hifadhi ya Serengeti na wananchi wanaoizunguka kwa kuwa wamekuwa wakivamia na kujenga ndani ya hifadhi na wakati mwingine kuingiza mifugo.

Katika ziara yake hiyo ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la Serengeti, Mabula alifuatana na Mkuu huyo wa Wilaya ya Tarime pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Upimaji Vijijini kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Huruma Lugalla ambao kwa pamoja walijionea hali halisi ya mpaka wa Tanzania na Kenya na baadhi ya alama za mipaka zilizoharibika.



from MPEKUZI

Comments