Mpima Ardhi Amwaga Chozi Mbele Ya Waziri Lukuvi

Mpima Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Bwana Thobias Patrick amemwaga chozi mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maeneleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akijitetea kuhusu tuhuma za kupima eneo la serikali na kujimilikisha kisha kuliuza.
 
Hayo yametokea jana wilayani Kahama mkoani Shinya wakati wa ziara ya Waziri Lukuvi katika kampeni yake ya Funguka kwa Waziri ambapo wakazi wa mji huo walimfikishia Waziri wa Ardhi tuhuma zinazomkabili afisa huyo.
 
Mara baada ya kupata tuhuma hizo Mhe. William Lukuvi alitembelea eneo linahusishwa na tuhuma hizo na kumhoji afisa huyo kwanini alipima eneo la serikali na kumilikisha watu binafsi na yeye akiwa mmiliki wa kiwanja kimoja wapo na kisha kukiuza.
 
Mpima Ardhi huyo Bwana Thobias Patrick alipata wakati mgumu kujibu tuhuma hizo ambazo zimekuwa zikimkabili kwa muda mrefu hali iliyompelekea kutokwa na machozi huku akijitetea kuwa eneo linalohusishwa na tuhuma hizo sio la kwake kwakuwa yeye aliuza kiwanja namba 590 Block N na sio hicho anachotuhumiwa kukiuza.
 
Waziri Lukuvi alimuonya afisa huyo kutojihusisha na ununuzi wa maeneo yenye utata wakati akijua yeye ni mtumishi wa serikali tena akiwa afisa anayehusika na upimaji wa maeneo hayo.
 
Waziri Lukuvi yupo katika ziara zake za kukutana na wananchi walio na migogoro ya ardhi na kuitatua ana kwa ana.
 
Kwa sasa anaendelea na ziara yake kutatua migogoro ya ardhi katika kampeni yake ya Funguka kwa Waziri ambapo hadi sasa ameishasikiliza na kutatua kero na migogoro zaidi ya 2,000 katika Mkoa wa Dar es salaam na wilaya zake za Ilala, Kinondoni na Temeke na mkoa wa Kagera katika Wilaya za Karagwe, Kyerwa na Ngara na mkoa wa Shinyanga katika wilaya ya Kahama.
 
Kwa sasa Waziri Lukuvi anataraji kufanya ziara katika Mkoa wa Pwani ambapo kuna migogoro mingi ya ardhi ya muda mrefu na baadae kwenda wilaya nyingine katika kutekeleza kampeni ya “Funguka kwa Waziri” yenye lengo la kutatua migogoro ya ardhi katika wilaya zote za Tanzania bara.


from MPEKUZI

Comments