Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 03

Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam
Nilifikiri kuwa kwa kesi yake, angehitaji mchungaji au mtumishi wa Mungu mwenye nguvu na uzoefu wa kushughulika na nguvu za giza na nguvu za kichawi. Akiendelea kuongea, akilini alinijia kaka yangu mmoja ambaye ni mchungaji, nikakumbuka katika uzoefu wake wa kuombea watu wanaosumbuliwa na mambo mbalimbali amewahi kukutana na kesi za mapepo na wachawi mara kadhaa.

Lakini nilianza tena kuwaza kama muhusika angekubali habari yake aambiwe mtu mwingine yeyote. Mazungumzo yetu yalikuwa siri kubwa ambayo nina hakika hangetaka yajulikane kwa watu. Aliamua kuniamini mimi pekee, na kumjulisha mwingine kwake ilikuwa kama kuyaweka maisha yake hatarini.

Baada ya maongezi ya muda mrefu, huku nikimsikiliza neno kwa neno, nilianza kupangilia namna ya kumjibu. Nikachukua kama sekunde kadhaa nikitafakari, kisha nikamwambia, “Unaweza kuniamini?” Nilianza kwa kumuuliza, akanijibu ndio huku akionyesha kutafakari kwanini nimemuuliza hivyo.

Niliisoma akili yake ikijiuliza inakuaje namuuliza swali kama hilo ilhali tayari ameniamini sana na ndio sababu ya kuja kuongea na mimi. Ni kweli aliniamini, lakini nilimtaka aniamini zaidi ya hapo. Nilimtaka aniamini kwa maamuzi niliyotaka kuyafanya, aamini kwamba nitamuweka kwenye mikono salama ya mtu atakayeweza kumsaidia zaidi yangu.

Nilianza kumueleza kwa kirefu kuhusiana na kaka yangu ambaye ndiye mtu nilifikiria angemsaidia. Unajua hata inapokuja kwenye suala kama ajira, kabla ya kumuunganisha muajiri kwa mtu anayetafuta kazi, ni vema ukahakikisha ameelewa na kukubali vigezo vya huyo ambaye unataka aajiriwe kwanza. Sasa hapa ilikuwa ni zaidi ya kazi ya kuajiriwa, bali mustakabadhi wa maisha ya mtu, ilikuwa ni muhimu sana kwamba nimuunganishe na mtu ambaye sitamfanya ajutie kujiweka wazi kwangu. 



from MPEKUZI

Comments