Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 01

Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam
“Habari dada Grace! Ninaweza kuonana na wewe tuongee?”
Nilipata ujumbe huo mfupi wa simu kutoka kwa namba nisiyo ifahamu nikiwa katikati ya shughuli zangu.

Nilisoma nikajiambia kuwa ningempigia baadaye kujua ni nani na ni sababu gani hasa inamtaka aniombe tuonane. Simu yangu ya awali ilikuwa imeharibika hivyo kunifanya nipoteze baadhi ya namba, hivyo sikuwa na ujasiri sana wa kumuuliza mtu ni nani endapo ametumia namba nisiyoifahamu na hajajitambulisha.

Niliendelea na kazi zangu, nikarudi kwangu na kuwa bize na shughuli za ndani, nikaja kukumbuka ule ujumbe nikiwa kitandani tayari kwa kulala. Mara nyingi huwa sipendi kupiga simu ikishafika saa nne usiku, nikaamua kwamba ningempigia yule mtu kesho yake.

Asubuhi sana nikiwa ndio naamka uliingia ujumbe mwingine kwenye simu yangu, “Dada Grace, naitwa Jovina, hunifahamu ila mimi nakufahamu kwa kusikia habari zako. Nahitaji sana kuongea na wewe, najua utanisaidia.”

Nilimpigia muda huo na kumwambia juu ya ratiba yangu ya siku hiyo. Nilikuwa na muda kuanzia mchana na ingebidi anifate maeneo ambayo ningekuwa, kwa bahati akawa tayari kunifuata popote.

Alidai maongezi yetu yangechukua muda mrefu kidogo na yangehitaji sehemu tulivu. Nilimuomba tukutane maeneo ya chuo  kikuu cha mlimanii kwani huko tungepata sehemu tulivu bila kuingia gharama yoyote, na pia nilikuwa na kazi kadhaa za kufanya nikiwa huko chuo. Dakika kumi kabla ya muda niliopanga tuonane alinipigia, tukakutana.

Kwa muonekano huyu ni binti umri wa kati, siyo mdogo sana lakini sikudhani kama huenda akawa mwanamke mwenye watoto. Ni mzuri wa sura na rangi, mrefu kiasi na siyo mnene.

Hakuna mtu ambaye angemtazama na kuhisi mzigo alioubeba, kwani uso wake una tabasamu muda wote na ana muonekano wa kujiamini. Nilipoanza kumsikiliza ndipo niligundua kuwa alichobeba moyoni hakiwezii kuonekana kwa macho.

“Kuna siku nikiwa na mawazo mengi mno kuhusiana na hali ambazo nimekuwa nikipitia, niliamua kupitia mtandaoni, nikakutana na post yako ya ushuhuda ambayo rafiki yangu wa fesibuku alikuwa ameshea kwenye kurasa yake. Nilitazama picha yako ile uliyolala kitandani unaumwa kabla sijasoma, nikajikuta natoa machozi (mimi ni mtu wa machozi ya karibu sana).

Nilianza kusoma nikahisi ni hadithi au habari ya mtu mwingine kwani sikuamini kuwa mwenye hiyo picha inayoonekana ndiye aliyeandika hayo yote, kwani ulionyesha ni mwaka tu umepita.

Kuanzia hapo nilifuatilia huo ushuhuda wako mpaka mwisho na hakuna simulizi ya mtu imewahi kuniliza kiasi kile. Baada ya kukufuatilia kwenye kurasa yako, na ule ushuhuda wako, niliiambia nafsi yangu kuwa huenda wewe ukawa mtu sahihi kuongea naye.

Najua ninachokwambia huenda hakitahusiana sana na ushuhuda wako, lakini ndani ya nafsi yangu nimeona ni vema niongee na wewe, na nashukuru sana umekubali kunisikiliza.

Nina miaka 26, na nina mume na watoto wawili. Niliolewa nikiwa na miaka ishirini lakini ilikuwa kwa shinikizo la wazazi wangu. Mume wangu ana pesa nyingi mno, yaani ni Tajiri sana, lakini hutaweza kuamini maisha ambayo mimi na watoto wangu tunaishi.

Tunaishi maisha ya kawaida kabisa, usafiri tunaotumia ni daladala mara zote isipokuwa siku ambazo tunatoka na mume wangu. Yeye ana gari nzuri, za kifahari na siyo moja wala mbili lakini siruhusiwi hata kupewa dereva aniendeshe.

Ananipa mahitaji yangu yote lakini sina akaunti ya binafsi wala siwezi kupewa kiwango kikubwa cha pes hata siku moja. Wakati naolewa nilikuwa ndio nimemaliza diplopa ya mambo ya hoteli lakini sikuwahi kuruhusiwa kufanya kazi, ingawa niliona ni kawaida sababu mume ana pesa na hata kazi ambayo ningepata ingekuwa ya kipato kidogo tu, lakini nilipoingia kwenye ndoa niliona bora ningefanya hata kazi ndogo. Kwa sasa kiukweli hayo maisha nimeyazoea na najionea sawa tu.

Mume wangu aliwashawishi wazazi wangu kwa pesa zake kunioa, wakidhani wananipeleka kwenye mikono salama, lakini kumbe walikuwa wananipeleka kwenye uangamivu mkubwa.

Ndani ya miaka sita ya ndoa yangu nimekuwa mtumwa mkubwa Grace, nilikuja kugundua miezi michache tu baada ya kuolewa kuwa mume wangu ni mchawi na sharti kubwa la pesa zake ni mke wake asionekane hata siku moja kama mke wa tajiri. 

==>Endelea Nayo <<Kwa Kubofya Hapa>>


from MPEKUZI

Comments