Agizo alilolitoa Waziri Mkuu akiwa mkoani Mtwara Kuhusu Watoto Wenye Ulemavu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalumu kutowafungia ndani na badala yake wawapeleke shule.

Amesema ulemavu si kigezo cha kuwakosesha watoto hao kupata elimu na kufanya kazi, hivyo amewataka jamii kutowakatisha tamaa

Alitoa agizo hilo jana (Jumanne, Februari 27, 2018) wakati alipokagua mradi wa ujenzi wa majengo ya chuo cha Ualimu Kitangali, kilichopo Newala mkoani Mtwara.

“Watakaobainika kuwafungia ndani watoto wenye mahitaji maalumu wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu wanawakosesha haki ya kupata elimu.”

Pia amewaagiza watendaji wa vijiji wafanye sensa katika maeneo yao ili kubaini idadi ya watoto hao na watakapofikia umri wa kwenda shule wapelekwe.

Waziri Mkuu alisema Serikali inataka watoto wenye mahitaji maalumu watambulike pamoja na mahitaji yao na waliofikia umri wa kwenda shule wapelekwe.

“Tunataka kila mtoto wa Kitanzania aliyefikia umri wa kwenda shule apelekwe shule na kusoma na wenzake. Serikali imeboresha elimu ili watoto wote wasome”.

Alisema watoto wenye mahitaji maalumu wana haki sawa na wengine, hivyo hakuna sababu ya kuwafungia ndani na kuwakosesha kupata elimu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo alisema mradi huo unahusisha ujenzi na ukarabati wa vyuo vinne vya ualimu.

Dkt. Akwilapo alivitaja vyuo hivyo ni Ndala cha Tabora, Mpuguso cha Mbeya, Kitangali cha Newala na Shinyanga, ambapo ujenzi utagharimu sh. bilioni 36.47.

Alisema mradi huo wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo hivyo vinne utaleta tija kubwa kwa Serikali katika kuongeza fursa za kutoa mafunzo ya ualimu katika ngazi za stashahada na shahada.

“Vyuo vyote hivi vinne vitakapokamilika vitakuwa na uwezo wa kudahili wanachuo 3,300 kwa wakati mmoja kutoka uwezo wa sasa wa kudahili wanachuo 1,855”.

Akizungumzia kuhusu chuo cha Kitangali ambacho kilijengwa 1937, alisema kinajengwa upya kutokana na uchakavu wake kiasi cha kutofaa kufanyiwa ukarabati.

Awali, Kaimu Mkuu wa chuo hicho Mwalimu Emmanuel Haule alisema Serikali kwa kushirikiana na Canada zimetoa sh. bilioni 8.26 za ujenzi wa miundombinu.

Mwalimu Haule alisema miundombinu inayojengwa chuoni hapo ni pamoja na vyumba vya madarasa, mabweni, nyumba za watumishi na maabara.

“Pia tunajenga ukumbi wa mikutano na ukumbi wa mihadhara, maktaba na uchimbaji wa kisima cha maji. Ujenzi unatarajiwa kukamilika Aprili 26, 2018.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 28, 2018.


from MPEKUZI

Comments