Waziri Mkuu asema Afrika imeazimia kujiimarisha kuzalisha umeme

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema nchi za bara la  Afrika zimeazimia kujiimarisha katika uzalishaji wa umeme hadi vijijini ili uweze kuleta maendeleo.

Taarifa iliyotolewa leo Januari 30, mwaka 2018 na ofisi ya Waziri Mkuu imesema Majaliwa ametoa kauli hiyo jana Januari 29, 2018 baada ya mkutano wa viongozi wakuu wa nchi za Afrika uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Amesema nchi hizo zimeazimia kuzalisha umeme mwingi kwa lengo la kuinua kiwango cha maisha ya wananchi wake na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi

Katika mkutano huo ambao Majaliwa alimuwakilisha Rais John Magufuli, amesema nchi za Afrika zimejipanga kuzalisha umeme wa kutosha mijini na vijijini.

Amebainisha kuwa nchi hizo zinatakiwa zijitegemee kiuchumi, ambapo nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na jumuiya nyingine za Afrika zimefikia mapendekezo ya kuimarisha uzalishaji wa umeme.

“Tanzania iko vizuri kwa sababu ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme na sasa ina mikakati ya kuzalisha umeme wa kutosha kuendesha viwanda vikubwa na kukaribisha wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali,” amesema Majaliwa.

Katika hatua nyingine, Waziri  Majaliwa amesema malengo  ya mkutamo huo yalikuwa ni kupokea taarifa za tume mbalimbali zilizoundwa katika kikao kilichopita.

Amesema miongoni mwa taarifa hizo ni pamoja na ya tume iliyokuwa  inashughulikia masuala ya usalama na amani bara la Afrika.


from MPEKUZI

Comments